HabariHabari za Kitaifa

RUTO APAA: Ziara ya kwanza ya kimataifa kwa miezi miwili

Na  CHARLES WASONGA August 11th, 2024 1 min read

RAIS William Ruto ameondoka nchini kuelekea Rwanda katika ziara yake ya kwanza nje ya Kenya tangu vijana wa Gen Z walipoanzisha msururu wa maandamano kupinga sera za serikali yake hasaa Mswada wa Fedha wa 2024, mnamo Juni 18, 2024.

Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed Jumapili alitangaza kuwa Rais Ruto yuko jijini Kigali, Rwanda, kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais Paul Kagame kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa Julai 15.

“Rais William Ruto alisafiri kuelekea Kigali, Rwanda, Jumapili Agosti 11, 2024 kwa mwaliko wa Mheshimiwa Paul Kagame kuhudhuria kuapishwa kwake ili ahudumu kwa muhula wa nne afisini. Hii ni kufuatia ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa Julai 15,” Bw Hussein akasema.

Bw Kagame aliapishwa Jumapili, Agosti 11, 2024 baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi huo kwa kupata asilimia 99.9 za kura zilizopigwa.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 66 aliwania kwa tiketi ya chama tawala cha Rwanda Patriotic Front (RPF) na kuwashinda wapinzani wake wawili,

Frank Habineza wa chama cha Democratic Green Party of Rwanda na mgombea huru  Philippe Mpayimana.

Rais Ruto ni miongoni mwa marais 20 wanaohudhuria hafla hiyo ambayo pia inahudhuriwa na zaidi ya watu 40,000.

Tangu Juni 18, 2024, Dkt Ruto alipositisha ziara nje ya nchi, alikuwa amezuru jumla ya nchini 36 ndani ya muda wa miezi 20 tangu alipoingia afisini Septemba 13, 2022.