Habari za Kitaifa

Huenda mashirika ya umma yakaishia kugharamia ukaguzi wa matumizi ya fedha

Na COLLINS OMULO September 9th, 2024 2 min read

HUENDA asasi za umma zikalazimishwa kugharamia shughuli za ukaguzi wa namna zilivyotumia fedha za umma, endapo zitawasilisha kuchelewa stakabadhi hitajika kwa maafisa kutoka Afisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali Nancy Gathungu.

Haya yanajiri baada ya wabunge kulalamika kuwa asasi za umma, hasa serikali za kaunti, hufeli kuwasilisha stakabadhi hizo kwa wakaguzi na kufanya hivyo kwa kamati za bunge wakati wa uchambuzi wa ripoti za ukaguzi.

Wabunge wamekubaliana na ombi la Bi Gathungu kwamba wabuni sheria itakayolazimisha asasi za umma kugharamia shughuli zote za ukaguzi wa baadaye.

Alipofika mbele ya Kamati ya Seneti Kuhusu Uwekezaji na Hazina Maalumu (CPAIC), Ijumaa wiki jana, Bi Gathungu alisema baadhi ya asasi 12, 000 za umma ambazo hukaguliwa na afisi yake zimekuwa zikihujumu shughuli hiyo kwa kutowasilisha stakabadhi hitajika wakati zinapohitajika.

Hali hiyo, akasema, inalenga kulemaza shughuli ya ukaguzi wa matumizi ya fedha za umma katika asasi hizo.

Bi Gathugu alifichua kuwa nyakati zingine, wakazi kutoka afisi yake husibiri stakabadhi hizo kwa zaidi ya wiki moja ilhali wao hupewa muda wa majuma matatu pekee kukamilisha shughuli hiyo.

Kwa hivyo, kucheleweshwa kwa stakabadhi hizo huingilia muda wa maafisa hao wa kumaliza kibarua hicho kwa wakati.

Bi Gathungu aliahidi kuwasilisha bungeni ripoti ya asasi za umma zinazohujumu mchakato wa ukaguzi wa matumizi ya fedha za umma.

“Ikiwa tutalazimika kurejea tena kufanya ukaguzi, basi mteja ndiye atabeba gharama. Kwa hivyo, tunauliza bunge kutusaidia kufikia hili kwa kuunda sheria mahsusi kuifanikisha. Wakaguzi hutegemea stakabadhi kuendesha kazi zao na sio mambo mengine. Stakabadhi zote zinafaa kuwasilishwa kwa muda,” Bi Gathungu akaiambia kamati hiyo ya CPAIC inayoongozwa na Seneta wa Vihiga Godffrey Osotsi.

Seneta wa Narok Ledama Olekina alikubaliana na pendekezo la Bi Gathungu akisema wameshuhudia malumbano kati ya magavana na wakaguzi kuhusu suala hilo la kuwasilishwa kwa stabadhi hitajika, kuchelewa na hivyo kuhujumu shughuli hiyo.

“Mara nyingi magavana hudai waliwapa wakaguzi stakabadhi, nao wakaguzi hudai kutozipokea,” akasema Bw Olekina

Seneta wa Migori Eddy Oketch akaongeza: “Nadhani hii ni kizingizio cha nia mbaya kutoka kwa magavana. Tungependa afisi yake itupe ratiba ya mawasiliano kati ya afisi yako na wateja kila baada ya kukamilika kwa shughuli ya ukaguzi.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti Bw Osotsi alikubaliana na Bi Gathungu akisema wakaguzi hawafai kushughulikia suala lolote pale stakabadhi zinapowasilishwa kuchelewa.

“Suala lolote la ukaguzi linapasa kushughulikia ndani ya muda wa ukaguzi sio nje ya muda huo,” akasema Seneta huyo wa Vihiga, ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa ODM.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga