Habari za Kitaifa

Serikali yatimiza ahadi kwa Raila kwa kupeleka rasmi jina lake kuwania kiti cha AUC

Na HARRY MISIKO July 30th, 2024 2 min read

NI rasmi sasa kwamba Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga atawania wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) Februari mwaka ujao.

Hii ni baada ya serikali ya Kenya Jumatatu kuwasilisha rasmi jijini Addis Ababa, Ethiopia, ombi lake la kutaka kushiriki kinyang’anyiro hicho.

Ombi hilo liliwasilishwa na Katibu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni Korir Sing’oei kwa Afisi ya Mshauri wa Kisheria wa Umoja wa Afrika (AU), kupitia msimamizi wa Eneo la Mashariki mwa Afrika Dharmraj Busgeeth, ambaye pia ni Balozi wa Mauritius.

“Chini ya mamlaka ya serikali ya Kenya na kulingana na Sheria na Kanuni za Tume ya Umoja wa Afrika, leo tumewasilisha stakabadhi za mteule wa Kenya kwa wadhifa wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mheshimiwa Raila Amolo Odinga,” Dkt Sing’oei akasema kwenye taarifa.

“Uamuzi huo unatokana na sifa za Bw Odinga kama mtetezi sugu wa masilahi ya Afrika, ufaafu wake, ufahamu alionao kuhusu masuala kuhusu mataifa mbalimbali na uwezo wake wa kuongoza AUC ambayo ni asasi kuu katika Umoja wa Afrika,” akaongeza.

Katika ombi lake, Bw Odinga ameelezea maono yake kwa AUC yanayohimiliwa katika nyanja mbalimbali zikiwemo; utangamano wa Afrika, ustawishaji wa miundo msingi, ustawi wa kiuchumi, kuendelezwa kwa biashara baina ya mataifa ya Afrika, kujitegemea kwa Afrika kifedha na nyanja za usawa wa kijinsia.

Nyanja zingine katika maono ya Bw Odinga ni maendeleo ya sekta ya kilimo, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Amani na Usalama na uwezeshwaji wa vijana.

“Bw Odinga atatoa kipaumbele kwa mchakato wa matumizi ya utajiri wa rasilimali ya kibinadamu na kiasili zilizoko Afrika ili kuiweza bara la Afrika kufikia upeo wa ufanisi. Analenga kuigeuza Tume ya Umoja wa Afrika ili iweze kuandikisha ufanisi kwa manufaa ya bara letu,” Dkt Sing’oei akasema.

Miongoni mwa stakabadhi zilizowasilishwa jijini Addis Ababa ni Wasifu Kazi wa Bw Odinga, uliotafsiriwa kwa lugha sita zinazotambuliwa na AU, kulingana na hitaji la Afisi ya Mshauri wa Kisheria katika umoja huo.

Lugha hizo ni; Kiswahili, Kiingereza, Kiarabu, Kifaransa, Kireno na Kihispania.

Kuwasilishwa rasmi kwa ombi la Bw Odinga sasa kumeondoa dukuduku kuhusu kujitolea kwa Rais William Ruto na serikali yake katika kumuunga mkono kiongozi huyo wa upinzani kwa wadhifa huo.

Awali, serikali ilikuwa imeahidi kuwasilisha rasmi ombi hilo, na stakabadhi hitajika, kabla ya Juni 30, mwaka huu.

Hata hivyo, ilifeli kutimiza ahadi hiyo na hivyo kuibua wasiwasi kuhusu kujitolewa kwa serikali kumuunga mkono Bw Odinga.

Hata hivyo, muda rasmi wa makataa ni Agosti 7, mwaka huu.