Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Msichana ameniarifu anapendana na mpenzi wangu

May 30th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nimekuwa na mpenzi kwa miaka miwili na nampenda sana. Kuna msichana aliyenitumia SMS juzi akaniambia kuwa mwanamume huyo ni mpenzi wake. Nilimuuliza mpenzi wangu akaniambia kuwa hana mwingine ni mimi tu. Nilimtumia ujumbe wa msichana huyo na nikamwambia sitakubali anichezee. Siku iliyofuata alinitumia SMS akaniambia nikome kuwasiliana naye kwa sababu amepata mwingine. Ajabu ni kuwa amekuwa akiwaambia marafiki zake kuwa ananipenda sana lakini hataki kuongea nami. Nampenda sana na sitaki kumpoteza. Nishauri.

Kupitia SMS

Kwanza, ulifanya makosa kumwamini msichana aliyedai kuwa mpenzi wa mpenzi wako. Inawezekana kuwa anammezea mate mpenzi wako na anatafuta mbinu ya kuwatenganisha ili amnyakue. Inaonekana mpenzi wako alikasirika kutokana na matamshi yako yaliyoashiria kwamba si mwaminifu kwako na hasira hizo ndizo zilizomfanya akwambie kuwa ana mwingine. Bila shaka hiyo si kweli na ndiyo maana anashikilia kuwa ni wewe tu anayependa. Ni muhimu umtafute umuombe msamaha ili kutuliza hasira zake na kufufua uhusiano wenu.

 

Ameniacha ghafla bila kunijulisha sababu

Shangazi pokea salamu zangu. Natumai wewe ni mzima. Nina mpenzi ambaye nampenda sana na tumekuwa pamoja kwa miaka miwili sasa. Sijui amefikiria nini kwani sasa ananiambia hataki tuendelee na uhusiano na nikimuuliza sababu haniambii. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Uhusiano, uwe wa kirafiki au wa kimapenzi ni chaguo la mtu binfasi na hakuna mikataba inayotiwa saini kudumisha mahusiano kama hayo. Inaonekana mwenzako amehisi kuwa hafurahii uhusiano wenu na ameamua kujiondoa. Hiyo ni haki yake na huwezi kumlazimisha kubakia katika uhusiano huo. Heshimu uamuzi wake na uendelee na maisha yako.

 

Kijana anataka tuwe wapenzi na bado ningali shuleni

Tafadhali nahitaji ushauri wako. Mimi ni msichana mwanafunzi wa shule ya upili na nina umri wa miaka 18. Kuna kijana ambaye amekuwa akinisumbua akitaka tuwe wapenzi lakini mimi nimeamua kujiepusha na jambo hilo hadi nimalize masomo. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni jambo muhimu sana kwamba unatambua kuwa masomo ndiyo unafaa kuzingatia kwa sasa wala si uhusiano wa kimapenzi. Kama wewe pia unampenda, mwambie wazi kuhusu uamuzi wako na umwambie asubiri.

 

Nina umri wa miaka 19, sasa nimeanza kushuku mpenzi aliye mbali

Shikamoo shangazi. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 19 na nina mpenzi ambaye nampenda sana. Hata hivyo anaishi mbali nami na nimekuwa nikishuku labda ana mwingine. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Hujaelezea ni kwa nini unamshuku mpenzi wako. Kama huna sababu nzuri, tosheka moyoni mwako kuwa ni mwaminifu kwako na hana mwingine. Ninashuku kuwa hali yako hiyo inatokana na ule wivu wa kawaida katika mapenzi na pia kwa sababu mpenzi wako anaishi mbali nawe.

 

Nilimtema ila sasa ataka turudiane, nipe ushauri wako

Kwako shangazi. Niliachana na mpenzi wangu siku wakati fulani aliponikasirisha sana. Sasa ananisumbua akitaka turudiane. Nishauri.

Kupitia SMS

Unafaa kuzingatia mambo mawili kuamua iwapo mtarudiana au la. Kwanza ni kitendo gani alichokutendea hadi ukakasirika. Je, uko tayari kumsamehe. Pili ni iwapo bado unampenda. Kama unampenda na uko tayari kumsamehe, basi fanya hivyo.

 

Nina wasiwasi ana mpango wa kando, nikimuuliza huwa anakasirika

Shangazi pokea salamu zangu. Nina mpenzi ambaye tunapendana sana ila nahofia kwamba ana mpango wa kando. Lakini kila nikimuulza hukasirika sana. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, unashuku tu wala huna hakika kwamba mpenzi wako ana mpango wa kando. Kama una hakika ya hilo, basi achana naye. Kama huna hakika, subiri hadi utakapokuwa nayo ndipo uchukue hatua inayofaa.