Makala

‘Shosho’ mkulima anayetumia You-Tube kusaka soko la mazao

May 18th, 2024 2 min read

SAMMY WAWERU Na LABAAN SHABAAN

MONICA Makokha mwenye umri wa miaka 56 angali na kumbukizi hai ya kuachwa na mume wake mpendwa katika umri mdogo mnamo 1994.

Ni mtu anayethamini familia na tangu udogoni alimwomba Mungu ampe ndoa yenye furaha.

Lakini kifo kilimpokonya mpenzi wa maisha yake akiwa na umri wa miaka 26.

“Niliachwa na watoto watano ambao sasa ni vijana,” Bi Monica anafichua akieleza kuwa baadhi yao tayari wameolewa.

Vile vile, Bi Makokha amemchukua mtoto mwingine kwa malezi – aliyeachwa yatima baada ya dada yake (mama mtoto) kufariki.

Baada ya kifo cha mume wake, Bi Monica ambaye ni mama mchangamfu na mchapakazi aliachwa hoi.

Monica Makokha akiwa kwenye shamba lake la maharagwe asilia Kakamega. PICHA|SAMMY WAWERU

Lakini ilibidi ajikung’ute mavumbi na kusimama tena ili aitunze familia yake.

Anasema hakuwa na jingine ila kujipa ujasiri wa kutosha kuwa nguzo ya familia, ambayo katika jamii nyingi inanyanyapaliwa.

Kuna jambo moja ambalo anamsifia marehemu mumewe kwalo –   msingi wa kilimo aliouweka.

“Ijapokuwa alikuwa ameajiriwa, alijishughulisha kikamilifu na ukulima nami nilimuunga mkono,” anasema.

Miaka 30 baadaye, Bi Makokha ni mmoja wa wanaothaminiwa katika Kaunti ya Kakamega kwa kudumisha utoshelevu wa chakula.

Shamba lake la ekari 10 katika kijiji cha Buchifi, Etenje, Mumias Magharibi, lina mazao yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi.

Miongoni mwa mimea anayokuza ni viazi vitamu, mihogo, nduma, mahindi, maharagwe, mboga za kiasili kama vile managu, mchicha na kunde.

Monica Makokha akionyesha maharagwe aina ya mucuna anayolima kudumisha afya ya udongo. PICHA|SAMMY WAWERU

Mjane huyo amekumbatia teknolojia za kilimo hai ili kupunguza matumizi ya kemikali.

Kilimo chake kimejikita katika teknolojia ambayo inahifadhi afya ya udongo ili kudumisha rutuba (regenerative agriculture).

Mbinu hii huhusisha kupunguza uvurugaji wa udongo kwa kutolima sana, kufunika shamba kwa majani ili kuhifadhi unyevuunyevu, kubalisha mimea inayopandwa shambani, kuchanganya mimea na misitu na kadhalika.

Bi Makokha pia huongeza thamani katika mazao kutengeneza unga wa viazi vitamu, ambao pia huchanganywa na bidhaa nyingine kutumia mtambo wake wa kusaga nafaka.

Kilimo ni chanzo kikubwa cha kumwezesha kulea na kuwalipia karo watoto.

Monica Makokha pia hukuza ndizi Kakamega na hutumia You-Tube kusaka soko la mazao. PICHA|SAMMY WAWERU

Na kwa sababu ufikiaji wa masoko ni changamoto kwa wakulima wengi, Bi Monica amekumbatia matumizi ya teknolojia ya kisasa na mitandao ya kijamii kutafuta wateja.

Hata katika uzee wake, anaendesha chaneli ya YouTube inayoitwa Monica Mkulima.

“Kuna wakati nilikuwa na ziada ya maharagwe maarufu njahi na niliuza yote kupitia chaneli yangu ya YouTube,” aliambia Taifa Dijitali wakati wa mahojiano shambani mwake Kakamega.

Miaka miwili baada ya kuzindua chaneli hiyo, Bi Monica anajivunia hatua hiyo.

Pamoja na maendeleo ya mtandao, wajasiriamali wengi wakiwemo wakulima, wametumia mitandao ya kijamii kuuza bidhaa zao.

YouTube, Facebook, Instagram na TikTok ndiyo majukwaa makuu ambayo mkulima huyu hutumia kuvumisha kazi yake.

Mkulima Monica Makokha akionyesha mhogo aliovuna shambani mwake Kakamega. PICHA|SAMMY WAWERU