Makala

Shule ya Hillside Endarasha yabadili sura kuondolea wanafunzi mafadhaiko


MMILIKI wa Shule ya Msingi ya Hillside Endarasha Academy iliyokumbwa na mkasa wa moto ulioua wanafunzi 21 amevunja ukimya.

Bw David Kinyua Wambugu anafunguka kuwa angali anahuzunishwa na janga hilo huku akitoa rambirambi kwa walioathiriwa katika mkasa huo wa Septemba 5, 2024.

“Nimeathiriwa sana na tukio hili kwa sababu sikuwa ninatarajia. Nimekaa na watoto miaka 13 na tumezoeana nao. Hata mimi nimehuzunika sana,” alisema kwa masikitiko.

Wiki mbili baada ya mkasa huo, mikakati ya kukarabati shule imeanza ili kupanga marejeleo ya masomo kabla ya mitihani ya gredi ya sita ya KPSEA mwezi Oktoba 2024.

Ukarabati huu shuleni umeanza baada ya Idara ya Upelelezi wa Jinai DCI kuikabidhi rasmi shule hiyo kwa uongozi wa wake baada ya kufungwa ili kupisha uchunguzi wa mkasa huo.

Huu ni mwanzo wa maandalizi ya kufunguliwa tena.

“Tumehamisha bweni na tunataka kulipeleka kwingine,” alisema Bw Kinyua. “Tunabadilisha njia ambayo, hasaa wavulana, walikuwa wanapitia ili wasiwe na kiwewe wanapopita wakiwa shuleni.”

Kadhalika, msimamizi wa shule ya Hillside anaeleza kuwa watapunguza idadi ya wanafunzi wanaolala shuleni kwa asilimia hamsini pindi tu shule hiyo itakapofunguliwa.

Bw Kinyua analenga kufungua ukurasa mpya wa tathmini akiangazia iwapo kuna kosa kuwahifadhi wanafunzi wengi zaidi ya 350 katika bweni moja.

Uchunguzi waendelea

Kulingana na Kaimu Kamishna wa Eneo la Kati, Pius Murugu, serikali itakamilisha uchunguzi wake kuhusu janga hilo wiki ijayo.

“Matokeo ya uchunguzi yataambatanishwa na mfumo wa utambuzi wa chembechembe za nasaba (DNA),” alieleza. “Sasa kuna jopo la wizara ya elimu linaloshughulikia ufunguzi wa shule hii.”

Kufikia wakati huu, ni wanafunzi wawili tu walioathiriwa na moto shuleni humo wamelazwa hospitalini kwa matibabu.