2027: Mawaziri watumia kandanda kujipanga?
NA WANDERI KAMAU
JE, huenda mawaziri katika serikali ya Rais William Ruto wameanza mikakati ya kujitayarisha kisiasa ielekeapo 2027 kupitia mashindano ya kandanda katika maeneo wanakotoka?
Hili ndilo swali kuu ambalo limeibuka kufuatia hatua ya mawaziri kadhaa kuzindua mashindano hayo.
Baadhi ya mawaziri hao ni Moses Kuria (Utumishi wa Umma), Susan Nakhumicha (Afya), Eliud Owallo (Habari, Mawasiliano na Teknolojia-ICT), Ababu Namwamba (Michezo) na Kipchumba Murkomen (Uchukuzi).
Mnamo Desemba 29, 2023, Bi Nakhumicha aliandaa makala ya nne ya Kombe la Nakhumicha katika Kaunti ya Trans Nzoia, ambapo timu iliyoibuka mshindi ilituzwa Sh500,000 huku ya pili ikiridhika na Sh300,000 nayo iliyomaliza katika nambari ya tatu ikienda nyumbani na Sh100,000.
Siku moja kabla, Bw Owallo aliandaa mashindano ya Eliud Owallo Super Cup, ambapo mshindi alituzwa Sh400,000 huku mshindi wa pili akipata Sh300,000.
Bw Namwamba na Bw Murkomen ni miongoni mwa mawaziri ambao wameandaa mashindano hayo katika maeneo wanakotoka—kaunti za Busia na Elgeyo Marakwet mtawalia.
Bw Kuria naye ametangaza kuzindua mashindano ya kandanda, anayoyataja kuwa “mkakati wa kuwakomboa vijana katika eneo la Mlima Kenya”.
Kulingana na tangazo alilotoa Jumamosi, Januari 6, 2024, Bw Kuria alisema kuwa mashindano hayo ya kandanda yatahusisha maeneobunge yote 64 katika ukanda huo.
“Mashindano haya ni ya kutoa mwelekeo na ushauri kwa vijana katika eneo hili,” akasema.
Ijapokuwa kuna mashindano mengi ya kandanda ambayo yamekuwa yakifanyika katika ukanda huo, kile kimezua msisimko ni kiwango kikubwa cha pesa ambacho washindi watatuzwa.
Kulingana na tangazo hilo, jumla ya Sh9 milioni zitashindaniwa.
Mshindi atazawadiwa Sh5 milioni, atakayeibuka wa pili akijishindia Sh3 milioni, huku timu itakayoshikilia nafasi ya tatu ikizawadiwa Sh1 milioni.
Timu zitakazoshiriki zimegawanywa katika makundi manane.
Mashindano hayo, ambayo yataanza Februari 4, 2024, yatazishirikisha kaunti za Kiambu, Murang’a, Nyeri, Laikipia, Nyandarua, Nakuru, Meru, Tharaka Nithi na Isiolo.
Ijapokuwa Bw Kuria amekuwa akifadhili baadhi ya timu za kandanda katika ukanda wa Mlima Kenya, kama vile Thika United, baadhi ya wadadisi wametaja mashindano hayo makubwa kuwa na “ujumbe fulani wa kisiasa”.
Wanasema kuwa kama waziri, mashindano hayo yataonekana kuwasilisha ujumbe fulani wa kisiasa.
“Haya si mashindano ya kawaida, hasa yanayofadhiliwa na mawaziri. Zaidi ya hayo, yanawahusisha vijana. Kuna ujumbe fiche wa kisiasa wanaowasilisha mawaziri hao, ambapo wengi ni wanasiasa,” asema Bw James Waithaka, ambaye ni mdadisi wa siasa.
Kulingana naye, kuna uwezekano, kwa mfano, Bw Kuria analenga kuimarisha uungwaji mkono wake miongoni mwa vijana katika ukanda huo ielekeapo 2027.
“Bw Kuria ni mwanasiasa. Kupitia semi na vitendo vyake, amekuwa akionyesha dalili za kutaka kutwaa uongozi wa Mlima Kenya au kujitayarisha kwa nafasi kubwa zaidi ya kisiasa kwenye uchaguzi ujao,” akasema Bw Waithaka.
Kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, Bw Kuria aliwania ugavana katika Kaunti ya Kiambu, japo akashindwa na gavana wa sasa, Bw Kimani Wamatangi.