Aladwa amezea cheo cha Kiongozi wa Wachache ODM, Bunge la Kitaifa
MBUNGE wa Makadara George Aladwa ndiye mbunge wa hivi punde wa ODM anayemezea mate wadhifa wa kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa.
Wadhifa huo utasalia wazi ikiwa mshikilizi wake sasa, Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, ataidhinishwa kuwa Waziri wa Kawi.
Bw Wandayi, ambaye pia ni Katibu wa Masuala ya Kisiasa katika ODM, mbunge Maalum John Mbadi na magavana wa zamani Ali Hassan Joho na Wycliffe Oparanya ndio viongozi wanne wa chama hicho cha upinzani walipendekezwa Rais William Ruto kuwa Mawaziri.
Jana, Bw Aladwa alisema kuwa endapo hatapewa cheo cha Wandayi, basi ODM imtunuku cheo cha mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho kujaza nafasi ya Bw Mbadi aliyependekezwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango ya Kiuchumi.
Akiongea jana katika Kanisa la Kianglikana la St Stephen, lililoko kando ya barabara ya Jogoo, Nairobi, mbunge huyo alijinadi kama mbunge wa ODM mwenye tajriba kubwa zaidi kisiasa.
“Nimehudumu kama mwenyekiti wa ODM Nairobi kwa zaidi ya miaka 10. Kando na hayo, mimi ndiye mtetezi sugu wa kiongozi wa chama hiki Raila Odinga. Kwa hivyo, ninahitimu kuteuliwa kama kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa au kile cha mwenyekiti wa kitaifa wa ODM,” Bw Aladwa akasema.
“Isitoshe, ninaweza kuhudumu kama naibu kiongozi wa chama kujaza nafasi ya moja ya ndugu zangu Hassan Joho na Wycliffe Oparanya,” Bw Aladwa akaongeza huku akiwa amezingirwa na wafuasi wake.
Mbunge huyo hata hivyo aliwasuta baadhi ya wabunge wa ODM ambao tayari wametawazwa kuwa washikilizi wa muda wa wadhifa wa Kiongozi wa Wachache Bungeni, akisema nafasi hiyo bado haijatangazwa wazi.
“Wadhifa wa kiongozi wa wachache bungeni bado unashikiliwa na Bw Opiyo Wandayi. Mwenzetu amependekezwa kuwa Waziri wa Kawi na hajapigwa msasa na bunge inavyohitajika kikatiba na kisheria. Kwa hivyo, ni makosa kwa baadhi ya wenzetu kujitangaza kuwa washikilizi wa wadhifa huo,” Bw Aladwa akasema.
Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambi na mwenzake wa Embakasi Mashariki Babu Owino, tayari wamejitangaza kuwa ndio wanafaa kumrithi Bw Wandayi.
“Kuanzia leo mimi ndiye kiongozi wa upinzani kwa sababu kuna watu ambao walikuwa upinzani na sasa wamejiunga na serikali. Lengo langu ni kuwapigania raia na ni uchungu sana kuwaona wenzangu wakijiunga na serikali,” akasema Bw Owino.
Bw Aladwa aliwakemea wanaodai Bw Odinga amewasaliti kwa kujiunga na serikali akisema kuwa msimamo wa kigogo huyo wa siasa za upinzani haufai kupingwa.
“Raila amesema kuwa kunastahili kuwe na mazungumzo kuhusu masuala yanayoibuliwa na Gen Z na tunamuunga mkono kwa hilo,” akasema Bw Aladwa.
Tafsiri na Charles Wasonga