Anne Nderitu kuidhinishwa kwa wadhifa wake wa msajili wa vyama vya kisiasa
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta amemteua Ann Nderitu kwa wadhifa wa Msajili wa Vyama vya Kisiasa nchini.
Kwenye taarifa kutoka Ikulu ya Rais iliyosomwa bungeni jana na Spika Justin Muturi, Bi Nderitu, ambaye amekuwa akihudumu kama kaimu Msajili wa Vyama vya Kisiasa, aliteuliwa pamoja na Florence Taabu, Makore Wilson Mohochi na Ali Abdullahi Surro ambao wanatarajiwa kuhudumu kama manaibu msajili wa vyama vya kisiasa.
Wanne hao sasa watapigwa msasa na Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria inayoongozwa na Mbunge wa Kangema Muturi Kigano.
“Kamati hii itachapisha majina ya wanne hao magazetini na kualika umma kuwasilisha memoranda zozote kuhusu wanne hao ambao wamependekezwa na Rais kushikilia nyadhifa hizo muhimu,” Bw Muturi akawaambia wabunge Jumanne.
Bi Nderitu amekuwa akihudumu kama kaimu msajili mkuu wa vyama vya kisiasa kwa miaka miwili sasa kwani aliteuliwa mnamo Agosti 10, 2018.
Mnamo Juni 2020, Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) ilichapisha majina ya watu 10 walioorodheshwa kusailiwa kwa wadhifa wa Msajili Mkuu wa Vyama vya Kisiasa baada ya kutuma maombi.
Tume hiyo pia ilichapisha majina ya watu 12 walioorodheshwa kusailiwa kwa nafasi tatu za manaibu wa msajili wa vyama vya kisiasa.
Bw Kigano alisema Bi Nderitu na watatu hao ambao walipendekezwa kuwa manaibu wake watapigwa msasa na kamati yake mwishoni mwa wiki ijayo.