Babu Owino akana kumtafuta Gachagua, asema anachotaka ni uongozi wa ODM
MBUNGE wa Embakasi Mashariki Babu Owino amekana madai ya kumtafuta aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kushirikiana naye kisiasa huku akiapa kuwa lazima achukue usukani katika chama cha ODM.
Bw Owino alisema umakinifu wake ni kusaka kura za jamii zote Nairobi ili awe gavana na hatajikita katika siasa za ukabila kufanikisha azma yake.
“Mimi sijamtafuta Rigathi na mwenyewe hajanitafuta. Viongozi lazima wawe na mtu wa kumlaumu, mbona viongozi wa ODM wanafanya kazi na Ruto ambaye aliwapokonya ushindi?” akauliza.
“Tusiwe watu wa kutilia manani mambo madogo madogo, tumakinikie kusaka kura. Hata Rigathi si mwanasiasa mkamilifu ila tuongeze kapu letu la kura tuwahi uongozi na kuwasaidia watu wetu,” akasema Bw Owino.
Alikuwa akiongea Jumanne wakati wa mahojiano na Ramogi FM inayopeperusha matangazo yake kote nchini kupitia lugha ya Kiluo.
Mwanasiasa huyo analenga kuwania ugavana Nairobi 2027 na kumekuwa na madai kwamba anaegemea mrengo wa upinzani unaoongozwa na Bw Gachagua na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka.
Aidha, Bw Owino ni kati ya wanasiasa waasi wa ODM ambao wanapinga ushirikiano wa chama na utawala wa Rais William Ruto.
Mbunge huyo anayehudumu muhula wa pili, alisema anataka apokezwe ODM na hivi karibuni atatoa mwelekeo kwa wafuasi wa chama.
“Hivi karibuni nitaitisha kikao na kutoa mwelekeo lakini kwanza lazima nipewe uongozi wa chama, hapo hakuna hiari. Tusiwe watu wa kumzungusha Oburu kila mahali bila kumakinikia afya yake kwa nia ya kuwazuia baadhi ya watu chamani,” alisema.
Akaongeza, “Sisi vijana ndio tuna nguvu za kusaka kura na tunafaa kuzunguka na kuja kwa Oburu kumwambia mahali tumefika. Kuna watu wanaozungusha Oburu kila mahali kutimiza maslahi yao ya kibinafsi na hao ndio hawatutaki,” akasema.
Huku vita vya ubabe vikiendelea ndani ya ODM, Bw Owino alisema sasa amejiandaa kukabiliana na wapinzani wake, hasa akiwakashifu Mbunge wa Homa Bay Peter Kaluma na Diwani wa Kileleshwa Robert Alai, kama wanaomvamia bila sababu zozote.
Bw Kaluma ni kati ya wanasiasa wa ODM ambao wamekuwa wakipinga vikali chama kutwaliwa na baadhi ya viongozi chipukizi, akisisitiza mwelekeo wowote unastahili kutolewa na Dkt Oginga.
Kuhusu kufarakana na Bw Alai, Bw Owino amedai kuwa hana shida na diwani huyo, ila anatumiwa na baadhi ya watu serikalini kumpiga vita.