Babu Owino: Sihitaji tiketi ya ODM kumng’oa Sakaja uongozini 2027
MBUNGE wa Embakasi Mashariki, Paul Ongili Owino, maarufu kama Babu Owino, amethibitisha kuwa atakuwa debeni mwaka wa 2027 kuwania kiti cha ugavana wa Nairobi hata kama ODM haitampa tiketi.
Akitambua hali yake ndani ya chama hicho kinachoongozwa na Raila Odinga na mvutano wa tiketi ya chama hicho kutoka kwa wagombeaji wengine, Bw Owino sasa anawazia njia mbadala, ikiwemo kuwania kama mgombea huru.
Akiwa na matumaini ya dhati, mbunge huyo anasema yuko tayari kuwapa wakazi wa Nairobi uongozi mbadala na kurejesha jiji hilo kwenye heshima yake ya awali.
Hata hivyo, Babu, ambaye kwa sasa anahudumu muhula wake wa pili kama mbunge wa Embakasi Mashariki, anakumbwa na changamoto kutokana na kudhoofika kwa uhusiano wake wa karibu na ODM, chama kilichomdhamini kuingia bungeni.
Katika mahojiano na Taifa Leo, mbunge huyo alihusisha hali hiyo na ukosoaji wake wa mara kwa mara kwa Serikali Jumuishi, akisema kuwa ataunga mkono tu serikali inayowahudumia wananchi.
“Ninakosoa Serikali Jumuishi kwa sababu ni jambo sahihi kufanya. Kama kiongozi, siwezi kuona makosa na kuyanyamazia hadharani au hata faraghani,” alisema Babu Owino.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa heshima yake kwa Raila, haijatetereka, na kwamba kuidhinishwa kwa Gavana Sakaja hakutamzuia kuwania ugavana wa Nairobi.
“Ninajua ODM haitanipa tiketi. Ninajua kwa sababu Sakaja aliidhinishwa pale Bomas ya Kenya. Lakini bado nampenda Baba. Najua sitapewa tiketi, lakini hiyo haina maana yoyote, kwa sababu ni wananchi ndio hupiga kura,” alisema.
Alisema hana hofu kuhusu yajayo katika siasa, akithibitisha kuwa atakuwa debeni iwe kwa tiketi ya ODM au kama mgombea huru, licha ya kuwa chama hicho kimemuunga mkono tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2017.
Mbunge huyo anaamini kuwa alifikia alipo sasa kutokana na juhudi zake binafsi, hasa alipokuwa kiongozi wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
“Babu Owino ni taasisi,” asema.
Anasema heshima yake kwa Bw Odinga iko juu sana, licha ya kutokabidhiwa nafasi yoyote ya kamati ndani ya Bunge la Kitaifa.
“Babu asipopewa nafasi yoyote kwenye kamati, hakuna shida. Kile ninachobeba ni kikubwa kuliko hicho. Babu akikosa kuungwa mkono, hakuna shida, kile ninachobeba ni kikubwa na wataona thamani yake siku itakapowadia.”
Aidha, anakubali haki ya kidemokrasia ya Bw Odinga kumuunga mkono kiongozi yeyote, akisema hilo halimsumbui maadamu bado yuko hai.
“Katika familia, baba anaweza kumpenda mtoto mmoja zaidi ya mwingine, lakini hilo haliwezi kunifanya nimchukie au nipate uchungu naye. Yeye ni Baba na namjua. Ni mtu ninayempenda daima, ni mtu niliyeamini kwake. Kwa hiyo hakuna tatizo. Lakini wakati ukifika, kile ninachobeba kitathaminiwa na dunia nzima.”
Kwa upande mwingine, anadai kuwa Gavana Sakaja ameshindwa kutekeleza wajibu wake, jambo linalompa motisha ya kumtoa mamlakani.
“Gavana huyu ataondolewa na Wakenya kwenye debe. Nitakumbukwa kama mtu aliyeleta mabadiliko chanya, aliyepeleka watoto shuleni, aliyejenga barabara zetu, na aliyetoa ajira kwa wakazi wa Nairobi na Wakenya kwa ujumla.”