Siasa

Dorcas Rigathi aonya wanasiasa Murang’a ‘yote ni bure bila kujuana na Mungu’

May 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

MKE wa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Pasta Dorcas Rigathi amewashauri baadhi ya wanasiasa wa Murang’a kwanza wautafute ufalme wa mbinguni na hayo mengine watazidishiwa.

Maneno ya Bi Rigathi Dorcas katika kaunti ambayo inaongoza katika mchakato wa kumtaka Rais William Ruto amfute kazi Bw Gachagua yalionekana kama ya kumtetea mumewe.

Ni katika Kaunti ya Murang’a ambapo kuna mirengo miwili hasidi, mmoja ukimpigia debe Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro aibuke kuwa kinara wa siasa za Mlima Kenya dhidi ya Bw Gachagua.

Katika mazishi ya marehemu Peris Muiyuro ambaye ni mama mkwe wa aliyekuwa mwaniaji urais mwaka 2013 Peter Kenneth, Bi Rigathi alikumbana ana kwa ana na baadhi ya wanasiasa wa kaunti hiyo.

Jeneza la marehemu Peris Muiyuro ambaye ni mama mkwe wa aliyekuwa mwaniaji urais mwaka 2013 Peter Kenneth. PICHA | MWANGI MUIRURI

Waliohudhuria mazishi hayo katika eneobunge la Gatanga mnamo Ijumaa walikuwa ni Bw Kenneth, aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi, aliyekuwa mbunge wa Mathioya Bw Peter Kimari, diwani Kamau wa Mweha, aliyekuwa mbunge wa Maragua Bw Elias Mbau na pia aliyekuwa katibu maalum Bw Joseph Wairagu.

‘Aliyechokoza’ Mke wa Naibu Rais hadi akawaelekezea wanasiasa hao hotuba ya mahubiri ni Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe aliyekiri kwamba hajaokoka.

“Mimi sijaokoka lakini si hoja kwa kuwa wa kulaumiwa ni mamangu ambaye hakunishinikiza niwe mfuasi kwa dini,” akasema Bw Murathe.

Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe akihutubu kwenye ibada kabla ya mazishi ya Peris Muiyuro. PICHA | MWANGI MUIRURI

Bw Murathe hata hivyo alisema kwamba huwa anashiriki mahubiri ya runinga “na huwa sichelewi kuyasikiliza”.

“Niko na uhakika kwamba ninaweza nikaanza uhusiano na kanisa hata katika hali yangu ya sasa,” akasema.

Bw Ngugi naye alisema anatamani kujipa ushirika wa karibu na Mungu Muumba wake hivyo basi atatia bidii kukaribia madhabahu.

Bw Kenneth alisema kwamba ana mapenzi na Mungu na huwa anapenda kushirikiana na wachungaji.

Mwendazake alisifiwa kama aliyekuwa na uhusiano wa moja kwa moja na Mungu wake katika Imani ya Ukiristo na hata katika awamu yake ya mwisho katika uhai, alikuwa akikiri kumpenda Muumba.

Wakati Bi Rigathi alisimama na kujitambulisha kama mzawa wa kijiji cha Ndunyu ya Chege kilichoko Kaunti ya Murang’a, aliwarejelea wanasiasa hao, akiwashauri wachunge wasipate yote lakini wakaukosa ufalme wa mbinguni.

Aliwataka wajiepushe na ufukara wa Imani na uhusiano na Mungu akisema “yote ni bure ukiwa huna Mungu ndani ya maisha yako”.

Aliwataka waumini wote hasa wanawake wajitume kuwaombea wanasiasa hao wote waliotangaza nia ya kuanza safari ya kujuana na Mungu.

“Nawahakikishia kwamba kukiri kwenu kuwa mngependa kuwa na uhusiano wa karibu na madhabahu na Mungu kwa ujumla, ndio msingi ambao tutatumia kuwaandalia maombi ya kuwatimizia ari yenu,” akasema Bi Rigathi.

Aliongeza kwamba “tutahakikisha kwamba sio tu kuwa karibu na madhabahu bali pia mtakiri kwamba Mungu ni Bwana na Mfalme wa yote na vyote”.

Pasta huyo alisema kwamba kwa sasa ameitikia wito wa maombi ya kumsihi Mungu awatimizie matakwa ya nyoyo zao na azitulize zikome mahangaiko ya kujuana na Mungu.