• Nairobi
  • Last Updated June 15th, 2024 1:54 PM
Gachagua aomba Uhuru waungane

Gachagua aomba Uhuru waungane

LUCAS BARASA Na MARGARET KIMATHI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua kwa mara nyingine tena amemuomba Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kuungana naye katika juhudi za kuunganisha eneo na Mlima Kenya.

Haya yanajiri huku Bw Gachagua akishambuliwa vikali na viongozi chipukizi kutoka eneo hilo.

Mnamo Jumanne, Bw Gachagua alimsihi Bw Kenyatta kujiunga naye kuleta umoja katika eneo hilo lililo na wapiga kura wengi.

“Nikiwa kiongozi anayeshikilia wadhifa wa juu kutoka eneo hili, kazi yangu ni kuunganisha viongozi wote wakiwemo wale waliounga Azimio. Tunapaswa kuweka siasa kando, tusameheane na kuungana. Hata mwana wetu Uhuru Kenyatta anapaswa kujitokeza, tuungane,” Bw Gachagua alisema akiwa Kianyaga akielekea kwa mazishi ya aliyekuwa mwalimu wake Julius Kano Ndumbi.

Akizungumza kwa lugha ya Kikuyu, Bw Gachagua alisema kipindi cha kampeni kilipita na viongozi wanapaswa kuacha siasa kwa kuwa viti vya kisiasa huwa vya muda.

Bw Gachagua alisema kwamba, viongozi wanafaa kuungana na kufanyakazi na kuacha kumbukumbu nzuri.

“Umoja wetu ndio nguvu yetu, tunapokubali kugawanywa, basi tunapotea. Mlima wetu haufai kutumiwa katika siasa za nchi hii,” alisema.

Mchanganuzi wa masuala ya siasa, Prof Nyaga Kindiki anasema kwamba, Bw Gachagua hana chaguo isipokuwa kumtafuta rais mstaafu Kenyatta baada ya kutengwa na baadhi ya viongozi ili aweze kujijenga kisiasa.

“Hata hivyo, huenda naibu rais asifaulu kwa kuwa meli ya Kenya Kwanza tayari imeondoka kituoni huku Kenya Kwanza ikiwa serikalini na inaweza kumtenga katika uchaguzi mkuu wa 2027,” alisema Prof Nyaga ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Moi.

Aliongeza: “Naibu rais alianza vibaya kwa kuwa na kichwa ngumu na kufananisha serikali na kampuni inayomilikiwa na wenye hisa na kumlazimisha rais kwamba, iwapo alitaka kukutana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, ni lazima awepo ilhali kiongozi wa nchi ni wa Wakenya wote. Vile vile, alianza kumshambulia Raila na Uhuru na kutazama mali ya uhuru ilipokuwa ikiharibiwa na hata kunyimwa walinzi. Hata rais anaweza kukosa imani naye.”

“Sasa, lazima Naibu Rais anyenyekee na kuongea vizuri kudhihirisha ni kiongozi wa kitaifa na kuvutia watu. Kwa kuwa katika siasa, hakuna maadui lakini ni maslahi tu na baada ya kutengwa katika eneo la Kati, ni lazima atafute mtu wa kumsaidia ili aweze kufaulu katika azma yake ya kuwa rais mnamo 2032,” Nyaga aliongeza.

Huku Rais Ruto akiwa amemvuta Bw Odinga na kumweka chini ya mbawa za serikali yake kwa kumpigia debe kuwa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika, Bw Gachagua hana jingine ila kumtafuta Bw Kenyatta ambaye anataka kujifufua kama msemaji wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya baada ya jina lake kutajwa katika kongamano la Limuru III kama kiongozi wa jamii ya Agikuyu.

Prof Nyaga asema Bw Kenyatta angali na ufuasi mkubwa katika eneo la Mlima Kenya baada ya familia yake kutoa marais wawili na kwa sababu ya utajiri wa familia hiyo, marafiki na watu wengi ambao imesaidia.

  • Tags

You can share this post!

Wakulima waliopoteza mazao kwa mafuriko kukosa fidia

Maangamizi ya halaiki yananukia Sudan, UN yaonya

T L