Gachagua apiga raundi Mlimani
NA MWANGI MUIRURI
NAIBU Rais Rigathi Gachagua anafanya ziara katika ngome yake ya kisiasa Mlima Kenya, akiwahimiza wenyeji kuwa na umoja na kutia bidii kazini.
Akihutubu Jumanne akiwa katika mtaa wa nyumbani kwa Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru akiwa njiani kuelekea Gichugu ambayo ni ngome ya Martha Karua ambaye ndiye alikuwa mshirikishi wa Kongamano la Limuru III, Bw Gachagua alisema “umoja na bidii hufukuza umaskini na madharau.”
Kongamano la Limuru III lililoandaliwa katika Kaunti ya Kiambu mnamo Mei 17, 2024, na kuhutubiwa na wengi wa wakereketwa wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya wa kutoka ukanda wa Mlima Kenya, lilimlenga Bw Gachagua kama aliyezembea katika kutetea masilahi ya wenyeji.
Pia, Bi Waiguru katika siku za hivi karibuni ameashiriwa na baadhi ya wadau wa kutoa maoni kama aliye na pingamizi na mtindo wa utendakazi wa Bw Gachagua.
Lakini Bw Gachagua aliyekuwa safarini kuelekea katika eneo la Gichugu ambako ni nyumbani kwa Bi Karua alisimama mjini Kagio ambako ni hatua chache kutoka nyumbani kwa Bi Waiguru na akahutubia wenyeji.
“Mimi nimeamua niwatembelee kidogo nikiwa njiani kuhudhuria mazishi ya mwalimu wangu aliyenifunza enzi hizo katika shule ya upili ya Kianyaga. Sina maneno mengi ila tu kuwahimiza muwe na umoja na bidii kazini,” akasema Bw Gachagua.
Mwalimu Julius Kano Ndumbi aliaga dunia hivi majuzi na mazishi yake yalipangwa kufanyika Jumanne (leo). Bw Gachagua alikiri kwamba urafiki wake na mwalimu huyo ulikuwa umedumu kufikia kiwango kwamba “alinipongeza kwa kufanikiwa kuwa Naibu Rais”.
Bw Gachagua aliongeza kwamba “maneno ni mengi lakini ujumbe wangu kwenu ni muwe wa kupalilia umoja kama jamii za Mlima Kenya na muwe na bidii ya mchwa katika masuala ya kiuchumi ndio tuhepe dharau za kisiasa na za kiuchumi”.
Bw Gachagua aliyeshangiliwa kwa dhati na wenyeji, alisema atarejea katika ziara rasmi isiyo ya majonzi.
“Leo tunapita tukielekea kwa mazishi lakini nitarejea nikiwa pamoja na viongozi wenu kuongea mambo ya umoja na maendeleo,” akasema.