Siasa

Gachagua asema itakuwa ‘nipe nikupe’, aomba usaidizi wa jamii ya kimataifa

January 13th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu wa Rais Rigathi Gachagua jana alitoa wito kwa jamii ya kimataifa iingilie kati kuzima ghasia anazodhani zinadhaminiwa na serikali dhidi ya upinzani.

Bw Gachagua aliyekuwa akihojiwa kwenye redio jana asubuhi, aidha alisema upinzani hautavumilia iwapo ghasia hizo zitaendelea akiongeza kuwa itabidi nao wajilinde.

“Mlima Kenya sasa tumekataa kuvumilia zaidi fujo zake. Nimevamiwa zaidi ya mara 15 na hakuna hata mtu mmoja amekamatwa na sasa wakazi wameapa kuwa hata wao watajilinda,” akasema.

Pia aliwakemea wahudumu wa matatu na wamiliki wa magari hayo ambayo alidai yanatumiwa kuwasafirisha wahuni Mlimani kuvuruga mikutano yake.

Mbunge huyo wa zamani wa Mathira alitangaza vita vikali dhidi ya Rais Ruto Mlima Kenya na kusema ataandaa misururu ya mikutano 60 ukanda huo Februari na Machi.

Kiongozi huyo wa DCP alisema serikali imepoteza umaarufu na sasa inatumia ghasia dhidi yao akisema iwapo kuna ushahidi upinzani unapanga fujo hizo basi, serikali ina vyombo vya usalama vya kufahamu hivyo na kuuchukulia hatua.

Alimshutumu Rais Ruto kwa kutoa ahadi kwamba wahuni hawangetumika na wanasiasa ilhali utawala wake unawavumilia.

“Sasa tunapambana naye jinsi anavyotaka na tutajilinda. Hawezi kutudhulumu kiuchumi tena kimwili na tunyamaze tu,” akasema.

Alifichua kuwa fujo hizo zinalenga kuwavunja moyo wafuasi wake wasijitokeze kushiriki kura za 2027 ili arejee madarakani.

“Kwa hivyo, jamii ya kimataifa lazima ifuatilie yanayoendelea kisiasa nchini kuelekea 2027,” akaongeza.

Alikuwa akizungumza katika kituo cha redio cha Kameme ambapo alisema dhana kuwa upinzani unatumia ghasia ili kusaka huruma kutoka kwa umma ni potovu na haina mashiko.

“Wakisema tunajivamia basi tuulize nani anamiliki vitoza machozi? Bunduki? Na huwa kuna magari ya polisi waliovalia sare pamoja wakiandamana na wahuni pamoja na magari ya polisi,” akasema.

Bw Gachagua pia alilaumu Tume ya Uchaguzi (IEBC) akidai ina uoga wala haiwezi kukosoa vitendo vya ghasia alivyodai vinadhaminiwa na utawala wa sasa.

“IEBC ilinyamaza wakati wafuasi wetu waliumizwa na kupigwa kwenye chaguzi ndogo za Novemba 29. Tume hii haiwezi kuandaa uchaguzi ambao ni wa huru na haki,” akasema Bw Gachagua.