Siasa

Gachagua atambua ‘Uhuru ni mtoto wetu’

February 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA CHARLES WASONGA

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amenyoosha mkono wa maridhiano kwa Rais Mstaafu Uhuru Kenyattta akisema hana kinyongo chochote naye na kwamba ni “mtoto wetu hapo Mlima Kenya”.

Akiongea Jumamosi wakati wa mazishi wa aliyekuwa mkuu wa polisi King’ori Mwangi eneo la Tetu kaunti ya Nyeri, Bw Gachagua alieleza kuwa siasa ziliisha na hana hamna uhamasa wowote kati yake na Bw Kenyatta.

“Nilikuwa nikitarajia kukutana na rafiki yangu rais wa zamani Uhuru Kenyatta. Nilitaka kumsalimu kwa sababu sijamwona kwa kipindi kirefu na nimwambia mambo ni shwari. Ni mtoto wetu hapa Mlima Kenya, tulitofautiana kidogo lakini hayo yameisha,” Bw Gachagua akasema.

Alikariri haja yay eye na Bw Kenyatta kusuluhisha tofauti zao akiongeza kuwa miaka ambayo wamefanyakazi pamoja.

Katika miaka ya nyuma, Bw Gachagua alikuwa mshirika wa karibu zaidi wa Bw Kenyatta kiasi kwamba alihudumu kama msaidizi wake.

Lakini katika kuanzia mwaka wa 2021 hadi 2022, uhasama wa Bw Gachagua na Bw Kenyatta ulijitokeza. Mnamo Februari 2022 Bw Gachagua alikamatwa na kushtakiwa kwa tuhuma za wizi wa kima cha Sh7.3 bilioni, pesa kutoka asasi mbalimbali za serikali kuu na zile za kaunti.

Wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu mwa Agosti 9, 2022, Bw Gachagua alitumia majukwaa mbalimbali ya kisiasa kumshtumu Bw Kenyatta kwa kuendesha njama ya kumwekelea kesi za ufisadi kwa lengo la kuzima nyota yake kisiasa.

Lakini kuanzia Novemba 2023, Bw Gachagua alilegeza msimamo wake mkali dhidi ya Bw Kenyatta.

“Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ni mtoto wetu kutoka hapa kaunti ya Kiambu. Alihutumu kama Rais wa nne . Tulitofautiana naye lakini hayo sasa yamepita. Amestaafu na kurejea nyumba na kutulia, tunaheshimu uamuzi huo na serikali ya Kenya Kwanza itampa heshima zake,” Bw Gachagua akasema Novemba 14, 2023, katika eneobunge la Lari, kaunti ya Kiambu.

Bw Kenyatta alifika mapema katika mazishi hayo marehemu King’ori lakini akaondoka kabla ya Bw Gachagua kuwasili.

Mbunge wa Tetu Geoffrey Wandetto alisema kuwa Bw Kenyatta aliomba radhi kuondoka mapema kwa sababu alikuwa ameratibiwa kuhudhuria hafla nyingine ya mazishi kwingineko.