Siasa

Gachagua atoka pangoni

May 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua ambaye alikuwa ametoweka kutoka hafla za umma kwa zaidi ya siku 10 na kuzua wasiwasi wa kisiasa, ametangaza kujitokeza hadharani Jumapili.

Bw Gachagua ametangaza kwamba atakuwa katika Kanisa Katoliki la Endarasha lililoko katika eneobunge la Kieni, Kaunti ya Nyeri.

Aliongeza kwamba ataandamana na washirika wake wa karibu ambao ni pamoja na mbunge wa Kieni Bw Njoroge Wainaina, Gavana wa Nyeri Bw Mutahi Kahiga, Seneta wa Nyeri Bw Wahome Wamatinga na pia Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Nyeri Bi Rahab Mukami.

Tangazo lake la kujitokeza hadharani la Jumamosi aidha lilisema kwamba ataandamana na viongozi wengine wa kitaifa.

Soma Pia: Maswali Gachagua akikwepa hafla muhimu za kitaifa

Bw Gachagua anajitokea huku ngome yake ya Mlima Kenya ikiwa imewaka moto wa migawanyiko na pia tetesi kali kwamba utawala wa Rais William Ruto umegeuka kuwa sumu kwao kwa sababu ya ushuru wa juu.

Katika kongamano la Limuru III lililoandaliwa na wakereketwa wa Azimio La Umoja-One Kenya wa kutoka ukanda wa Mlima Kenya, Bw Gachagua na Dkt Ruto walizomewa kwa kiwango kikuu wakisemwa hawana manufaa ya kujivuniwa katika eneo hilo.

Sasa, Bw Gachagua ambaye hufahamika kwa kunena akijibu kwa ufasaha na shabaha, anatarajiwa kuwajibu wote ambao wamemwelekezea maneno katika siku hizo amekuwa pembeni.