Gachagua atumwa kuendea cheti cha ndoa yake ya kisiasa na Ruto
NA MWANGI MUIRURI
ATHARI za Kongamano la Limuru III lililoandaliwa na wakereketwa wa Azimio La Umoja-One Kenya kutoka Mlima Kenya ambao waliteta kwamba utawala wa serikali ya Kenya Kwanza ikiongozwa na Rais William Ruto haujali maslahi ya eneo hilo, sasa zimeanza kujitokeza kupitia presha kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Baadhi ya wakereketwa hata wanasema Bw Gachagua anafaa kujiondoa serikalini.
Kwenye kongamano la Ijumaa, baadhi ya viongozi walidai wafanyakazi wa serikali kutoka Mlima Kenya wanazidi kufutwa kazi, mawaziri na makatibu wa wizara kutoka Mlima Kenya kunyimwa nguvu baada ya kuwekewa majasusi kutoka kona ya Dkt Ruto ili kuwazima kusaidia Mlima Kenya na pia kupata migao isiyoambatana na idadi yao Mlimani.
Baadhi ya wanasiasa wa Mlima Kenya wamemtetesha Bw Gachagua kwamba aliingiza eneo hilo ndani ya serikali ya William Ruto bila chama wala mkataba wa kimaelewano hivyo basi kuipa serikali ya mrengo wa Dkt Ruto makali ya kudunisha Mlima.
“Bw Gachagua ndiye wa kulaumiwa kwa kusaliti jamii nzima ambayo iliporomoshea kapu la Ruto kura zaidi ya asilimia 85 ya kura zao na kuchangia asilimia 47 ya ushindi wake lakini sasa tukibaki kuwa waathiriwa wa kulialia kunyanyaswa kwa ushuru dhalimu,” akasema Bw George Maara ambaye aliwania Useneta wa Kaunti ya Kiambu lakini akaangushwa na Bw Karungo wa Thang’wa aliye mamlakani kwa sasa.
Mnamo Jumamosi, mwenyekiti wa chama cha Jubilee katika Kaunti ya Kirinyaga Bw Muriithi Kang’ara aliambia Taifa Jumapili kwamba “shida zote zilizo katika eneo la Mlima Kenya kwa sasa zilisababishwa na Bw Gachagua”.
“Ungekuwa ni mrengo wa Azimio–ambao Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alikuwa ametupendekezea ukiwa na Bw Raila Odinga kama mwaniaji wa urais–ulishinda, basi hatungekuwa hivi kwa kuwa tulikuwa na chama cha Jubilee kikiwa ni chetu na mkataba wa maelewano ulikuwa umeafikianwa,” akasema Bw Kang’ara.
Akiongea mjini Murang’a mnamo Februari 12, 2024, Bw Gachagua alisema kwamba “sisi tuliingia ndani ya ushirika na Dkt Ruto hata bila kuandikiana chochote kwa kuwa yeye ni muungwana na ni wa haki”.
“Rais Ruto tulimwamini alivyo na ana nia njema nasi…hatukufanya makosa na hata 2027 tutamuunga mkono kikamilifu,” alisema Bw Gachagua alisema.
Gavana wa Nyeri Bw Mutahi Kahiga aliteta kwamba “katika siku za hivi majuzi kumeanza kuchipuka presha zisizofaa miongoni mwa wadau wa kisiasa eneo la Mlima Kenya wakimlenga Bw Gachagua”.
Kwa sasa, Bw Gachagua anapambana na ujio wa ukaidi wa baadhi ya wanasiasa wa eneo hilo wanaomtaka Rais Ruto amfute kazi katika uchaguzi wa 2027 na badala yake amteue Mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro.
Pia, Kuna mrengo wa Bw Kenyatta ambao uliandaa Kongamano hilo la Limuru III na ambao husisitiza kwamba Bw Gachagua sio mwakilishi au msemaji wa Mlima.
Seneta wa Nyeri Bw Wahome Wamatinga alisema kwamba “sisi tunafaa kuwa na chama chetu cha kisiasa na kisha tujadiliane kuhusu mkataba wa ushirika wetu kama Mlima Kenya ndani ya Kenya Kwanza Alliance”.
Alisema kwamba walioingia KKA wakiwa na vyama vyao na pia wakiwa na mkataba wa kimaelewano waliishia kuvuna vinono huku Mlima Kenya ukiwa kwa kona ya mafupa.
“Chama cha Amani National Congress chake Musalia Mudavadi, kile cha Ford Kenya cha Moses Wetang’ula, kile cha Maendeleo Chap Chap cha Alfred Mutua na pia cha PAA chake Amason Kingi ni mfano bora,” akasema Bw Wamatinga.
Alisema kwamba wote hao walikatiwa minofu ya vyeo vya juu serikalini licha ya kuleta kura chache katika kapu la ushindi wa Ruto.
Hata hivyo, Bw Gachagua amekuwa akiteta kwamba “tuko na cheo cha pili kwa nguvu serikalini, serikali yote tumejumuika kwa zaidi ya asilimia 40 na mambo bado”.
Aliyekuwa Gavana wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu alisisitiza kwamba alikuwa katika kampeni za Dkt Ruto kuchaguliwa lakini “nimekuja kuelewa kwamba tulikosewa na Bw Gachagua”.
“Kwa wakati huo wote tukizunguka mimi nilikuwa nikifikiria tuko na mkataba wa maelewano na pia chama cha UDA kingeishia kuwa na uwazi wa kugawa hisa za ushindi,” akasema Bw Waititu.
Alisema kwamba “tangu nigundue kwamba hatukuwa na mkataba huo nimejiondoa kutoka chama hicho”.
Alisema kwamba atasikilizana na Bw Gachagua wakati atatangaza pia kujiondoa kwake na kisha atangaze kwamba atawania urais mwaka wa 2027 na pia awe tayari kushindana na wengine kupata tiketi hiyo.
Mbunge wa Githunguri Bi Gathoni Wamuchomba alisema kwamba “sisi sasa tutamtambua tu yule ambaye atatangaza kuwania urais hapa Mlima Kenya”.
Alisema hakuna haja ya kuendelea kuwatwika watu wa Mlima Kenya wa kulisha ng’ombe ambaye anakamuliwa kwa jirani.
Aliyekuwa Spika wa Kaunti ya Kiambu Bw Stephen Ndichu alisema kwamba “kwa sasa sioni umuhimu wa Gachagua katika serikali hii kwa kuwa hana mamlaka yoyote ya kutusaidia”.
Alisema ni lazima Mlima Kenya uwe na mwaniaji wa urais “na ikiwa Gachagua hataki, basi ataenda nyumbani na huyo Rais Ruto au hata wakishinda wawe sio wetu kamwe”.