Siasa

Gachagua ashikilia msimamo wa kuunganisha jamii za Mlima Kenya

June 8th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amesisitiza kwamba hakuna yeyote aliye na uwezo wa kumwagiza akome harakati za kuunganisha watu wa jamii za Mlima Kenya.

Mnamo Juni 2, 2024, akiwa katika uwanja wa Amutala ulioko Kaunti ya Bungoma, Rais William Ruto alisisitizia viongozi haja ya kutokuwa na siasa za ukabila na badala yake wawe wa ‘kutangatanga’ katika kila pembe ya nchi ili kujifahamisha na yale hufanyika katika maeneo mengine.

Rais Ruto alisema siasa za kukita kambi katika eneo la nyumbani la wanasiasa hazifai katika ulimwengu wa sasa akisema kwamba “kufanya hivyo hata hakukusaidii wewe mwenyewe kama kiongozi kujinoa katika kutekeleza majukumu yako ya kitaifa”.

Bw Gachagua naye akiwa katika hafla ya uzinduzi wa shoo ya Bahati Empire ambayo ni ukumbi wa msanii Kevin Mbuvi almaarufu Bahati na utakaokuwa ukipeperushwa moja kwa koja kupitia jukwaa la Netflix alisema “hakuna vile unaweza ukaunganisha taifa kutoka juu ukielekea chini”.

Hafla hiyo iliyoandaliwa katika mkahawa wa Westwood jijini Nairobi ilimpata Bw Gachagua akisema kwamba “kabla uwe Mkenya uko na ulazima kujifahamishe kama uliye na kwenu ulikotoka na kuunganisha taifa kunafaa kuanzia kwa mizizi hiyo yako”.

“Kila mmoja wetu ana kwao na ana lugha yake ya mama na ikiwa sisi ni watu wa imani kwa mpango wetu wa ‘Bottom-Up’ basi tuanze kuunganisha taifa na Wakenya kutoka pale kwa familia nyumbani, twende kwa kijiji, wadi kisha tupande hivyo tukielekea kuunganisha Wakenya,” akasema Bw Gachagua.

Alisema kwamba hata aitwe mkabila, hatakoma kusisitiza kuhusu umuhimu wa jamii za Agikuyu, Aembu na Ameru (Gema) kuwa katika ule umoja wa kijamii ndio sasa waakishaungana wao wenyewe, wawazie kuhusu vile wataungana na Wakenya wenzao katika ngazi ya kitaifa.

“Watu ambao wanaongea kwa lugha moja ya mama huwa na mahitaji yao ambayo ni yao tu na yanafaa kujadiliwa kwa lugha ya mama. Nikihimiza jamii yangu tuongee lugha hiyo ili kujadili changamoto zetu sioni yule ambaye tumemkosea. Mtu aunganishe watu wa kwao, mimi niunganishe wale wa kwangu na wale wengine wa kwetu ndio hatimaye tukutane mbele tuongee mambo ya Kenya,” akasema.

Bw Gachagua alisema hatamsikiliza yeyote ambaye atajitokeza kusema kwamba :tunafaa kukoma kuunganisha jamii mashinani”.

“Hili nitalifanya kwa uwezo wangu wote bila aibu na bila kuhitaji ruhusa kwa kuwa hilo ni jambo la maana kwetu kama jamii na kama taifa,” akasema.