Gavana Otuoma atafuta washirika wapya baada ya kuzomewa nyumbani
NA HASSAN WANZALA
GAVANA wa Busia Paul Otuoma sasa anaonekana waziwazi akitafuta washirika wapya baada ya kukataliwa nyumbani alipozomewa na umati kwenye mkutano wa kuwasajili wanachama wapya wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM).
Mnamo Jumanne, Bw Otuoma alimtembelea Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi katika ofisi zake zilizoko Railways, Nairobi.
“Tumefanya mkutano na Gavana wa Busia Paul Otuoma ambapo tumejadili masuala mengi na mikakati ya kuwainua watu wa eneo la Magharibi mwa nchi na Kenya kwa ujumla,” akaandika Bw Mudavadi mnamo Jumanne kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter).
Bw Mudavadi alisisitiza haja ya ushirikiano kukabili changamoto zilizoko na kuhimiza haja ya umoja kwa manufaa na mustakabali mwema wa taifa la Kenya.
Matukio haya yanajiri siku chache tu baada ya Bw Otuoma kuona giza katika kaunti yake.
Matatizo yake yalianza Jumatatu mjini Busia kwenye hafla ambayo kiongozi wa ODM Raila Odinga na viongozi wengine walihudhuria.
Bw Otuoma aliyezoa kura 164,478 na kumbwaga Sakwa Bunyasi wa Amani National Congress (ANC) aliyezoa kura 92,144 katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, ameanza kupoteza uungwaji mkono.
Mahojiano mengi na baadhi ya wakazi wa Busia yanaonyesha kwamba japo hajachomoka wazi kutoka ODM, anahusishwa pakubwa na siasa zinazoegemea Kenya Kwanza, muungano unaoongozwa na Rais William Ruto.
Gavana huyo alikuwa anasimama kuthibitisha uanachama wake kwa ODM alipozomewa vikali.
Licha ya mkurugenzi wa mawasiliano wa ODM kutangaza kwamba Bw Otuoma alikuwa mwanachama nambari 32, umati uliendelea kumzomea.
Hali ilivyotulia, Bw Otuoma alihutubu lakini tena akazomewa na akamualika Naibu Kiongozi wa ODM Wycliffe Oparanya.
Lakini kabla ya Bw Oparanya kuchukua maikrofoni, Bw Odinga aliichukua akawatuliza wenyeji.
“Ninaelewa hasira zenu kwa gavana Otuoma. Nitazungumza naye kisha nije niwafahamishe kitakachokuwa kimejiri,” akasema Bw Odinga.
Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna mnamo Jumanne aliambia Taifa Leo kwamba jopokazi litabuniwa kutathmini kilichojiri Jumatatu mjini Busia.
“Haitakuwa haki nitoe kauli yangu kabla ya uchunguzi wa kina kufanyika,” akasema Bw Sifuna.
Naye Bw Otuoma alisema Jumanne kwamba akili yake haiko kwa siasa bali kuwatumikia wenyeji na wakazi wa Busia.
“Huu si wakati wa siasa bali ni wakati wa kuwatumikia watu walionichagua,” akasema Bw Otuoma.
Kwenye vurumai za Jumatatu, ilikuwa ni mguu niponye wakati baadhi ya watu kwenye umati walitoa mapanga na marungu kuwashambulia waliokuwa wakimzomea Bw Otuoma.
Pia kuna madai kwamba masaibu ya Bw Otuoma yanaongezeka kwa sababu uhusiano wake na mbunge wa Budalang’i Raphael Wanjala si mzuri.
Akiwa katika mkutano wa wajumbe wa ODM katika Taasisi ya Mafunzo ya Busia, Bw Odinga alikiri kwamba malumbano ya viongozi ndani ya chama yanakipaka tope.
Maelezo zaidi na Justus Ochieng na Rushdie Oudia