Siasa

Gen Z waliowania chaguzi ndogo walivyokumbana na uhalisia wa siasa za Kenya

December 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWAMKO mpya wa kisiasa uliibuka mwaka jana, Gen Z walipoandamana huku wengi wakitangaza wazi hamu ya kushiriki kikamilifu katika uongozi wa taifa.

Tangu wakati huo, baadhi ya vinara wa vuguvugu hilo wamejiunga na vyama vya kisiasa wakishika nyadhifa mbalimbali, huku wengine wakithubutu kuingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi.

Hata hivyo, kwa wengi wao waliogombea chaguzi ndogo za Novemba 27, safari hiyo imekuwa funzo chungu kuhusu uhalisia wa siasa za Kenya, ambapo wazee huamua hatima, ari hutafsiriwa kama upumbavu na siasa safi haina nafasi bila pesa.

Katika eneobunge la Kasipul, mojawapo ya maeneo yaliyoshindaniwa vikali, Jeazmin Aoko, mwenye umri wa miaka 26, alipata kura 26 pekee na kuibuka wa tisa.

Alimshinda mgombea mmoja tu aliyepata kura 17. Akiwa mgombea huru na mwanamke pekee katika kinyang’anyiro hicho, anasema hatakata tamaa.

“Nitakuwa kwenye kinyang’anyiro 2027. Huu sio mwisho wa safari yangu ya siasa,” alisema, akieleza kuwa kampeni yake ya kwanza ilikuwa somo muhimu.

Alisema kuwania dhidi ya wagombea wanaoungwa mkono wa vyama vikubwa kulikuwa changamoto kubwa, na kuwashawishi wapigakura wamwamini kama kijana wa kike kulihitaji jitihada zaidi.

“Waliniuliza maswali kuhusu umri wangu na kama nina uwezo wa kuongoza,” alisema Aoko.

Kutokana na ukosefu wa magari, alitumia pikipiki au kutembea, hatua ambayo ilimsaidia kugundua barabara duni na madaraja yanayohitaji ukarabati.

Mara nyingi alifika katika maboma na kuwakuta watoto pekee huku wazazi wakienda kwenye mikutano mikubwa ya kampeni wanakopata pesa za kuhongwa.

Katika Mbeere North, Lawrence Ireri mwenye umri wa miaka 30 aliyewania kwa tiketi ya Safina Party, alipata kura 100. Anasema kilichomwangusha zaidi ni ukosefu wa pesa.

“Nilikubalika na vijana na wazee, lakini pesa ndizo ziliamua. Sikuwa na uwezo wa kugawa fedha kama washindani wangu,” alisema.

Ireri alitumia Sh20,000 pekee katika kampeni nzima na alizunguka kwa baiskeli na kipaza sauti akiwarai wakazi kumchagua. Alisema 2027 atachagua chama chenye nguvu zaidi.

Katika eneo la Magarini, Amos Katana, 25 alishindana na wakongwe wa siasa waliokuwa na mitandao na pesa. Ingawa alipata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa vijana, ikiwa ni pamoja na mgombea Gen Z wa kiti cha Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Kilifi Fatuma Ramadhan, Katana alimaliza wa nne kati ya wagombea 10 akiwa na kura 192.

Alisema alitegemea michango ya kifedha na kutembea kwa miguu kwenye kampeni zake, huku akilalamikia wizi wa demokrasia kupitia hongo za waziwazi.

“Ukiuza demokrasia kwa anayelipa zaidi, sauti ya mwananchi hupotea. Mimi ninataka kuleta mabadiliko, kurejesha matumaini na kusukuma maendeleo ya kweli,” alisema.

Katika Wadi ya Chewani, Kaunti ya Tana River, vijana wawili, Pascal Wayu (26) na Zena Haluwa (24), waliingia kwenye kinyang’anyiro na ari kubwa lakini wakakumbana na uhalisia mgumu wa siasa za eneo hilo.

Kwa Wayu wa Agano Party, wapigakura hawakuficha chochote.

“Watu walisema wazi kuwa bila kuwapa chochote hawangefika mkutanoni,” alisema. Alipata kura 38.

Kwa Haluwa, hali ilikuwa ngumu zaidi. Akiwania kwa tiketi ya Democratic Party, alikumbana na unyanyapaa wa umri, jinsia na matusi, hasa kutoka kwa wanawake.

“Baadhi ya wanawake wakubwa waliniita malaya. Walisema niwe na mume na watoto kwanza,” alisema.

Alisema vijana wa kiume walimnyanyasa kijinsia na hawakutilia maanani ajenda yake.

Alipata kura 48, ambazo anachukulia kama msingi wa safari ndefu.“Watu 48 waliniamini na hilo ni jambo la kutia moyo. 48 zikiwa 480 mwaka 2027, ninaweza kushinda,” alisema.

Wote wawili walisema ubaguzi wa umri uliwazuia sana kwani wakazi wakubwa waliona vijana kama wasio na uzoefu.

Licha ya changamoto hizo, wamesema watarudi 2027 wakiwa na uzoefu zaidi, mikakati bora na uelewa wa mazingira halisi ya siasa.

Ripoti hii imeandaliwa kwa ushirikiano wa George Odiwuor, George Munene, Maureen Ongala na Stephen Oduor.