Siasa

Hatujamaliza hata miaka miwili, afoka Gachagua akikemea siasa za urithi

June 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

VITALIS KIMUTAI NA LABAAN SHABAAN

NAIBU Rais Rigathi Gachagua anataka wanasiasa wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) kusitisha siasa za urithi zinazoendelea.

Siasa hizi zinatokota na kutisha kuvuruga shughuli za serikali hata kabla ya kukamilika kwa miaka miwili tangu serikali ichukue hatamu za uongozi wa taifa.

Naibu Rais anaomba wabunge na viongozi wengine wamshike mkono Rais William Ruto ili afanikishe maazimio ya utawala wa Kenya Kwanza.

Haya yanajiri wakati ambapo kuna majibizano ya hadharani kati ya Bw Gachagua na baadhi ya wabunge wa eneo la Mlima Kenya na lile la Bonde la Ufa; maeneo ambayo ni ngome za serikali ya UDA.

“Hizi siasa za urithi hazina maana, hazisaidii, hazifai na zinaudhi,” Bw Gachagua alisema akiwa Kericho mnamo Jumamosi.

Bw Gachagua amesema kuwa yeye alikuwa nguzo ya kutegemewa katika serikali ya Ruto na Wakenya wanafaa kupuuza wanasiasa wasioamini falsafa ya UDA na wanaojikakamua kuvuruga chama.

 “Shughuli muhimu sasa ambayo viongozi wanafaa kuzingatia ni kusaidia Rais kutimiza malengo yake. Siasa za nani ataongoza nchi 2032 zinafaa kutupiliwa mbali kwa sasa,” Bw Gachagua alisema.

Akizungumza katika hafla ya kuchanga pesa kanisani PMCA, Kipkok, eneobunge la Soin Sigowet, Naibu Rais alisema Wakenya walitarajia mengi kutoka kwa serikali ya Kenya Kwanza na viongozi hawafai kupoteza muda kupitia siasa mbaya inayoweza kusababisha utengano miongoni mwa Wakenya.

“Hatuna haja ya kujihusisha katika siasa za urithi sasa. Tunafaa kukomesha siasa hizi sababu hata hatujatawala kwa miaka miwili na nusu,” Bw Gachagua alisema.

 “Tuna ajenda yetu kama chama na wale ambao hawako upande wetu wanafaa kutukoma. Tutakwama na mpango wetu na tutaongoza kutoka mbele tunapowaunganisha watu na kutekeleza malengo yetu,” aliongeza.

Akiwa katika hafla iliyohudhuriwa na Gavana wa Kericho Erick Mutai, Kiongozi wa Wengi Seneti Cheruiyot, Mbunge wa Soin Sigowet Justus Kemei, Mbunge wa Emurua Dikirr Johana Ngeno, Mwakilishi wa Kike Kericho Beatrice Kemei, aliyekuwa mbunge wa Mosop Vincent Tuwei na Spika wa  Bunge la Kaunti ya Kericho Patrick Mutai, Bw Gachagua alisema kuna haja ya umoja katika utawala wa Kenya Kwanza.

“Siasa ni mchezo wa hesabu. Hatuna kuondoa, tuna kuongeza kwa sababu tunalenga kupanua mrengo wetu,” Bw Gachagua alisema akisisitiza UDA inalenga kuvuma hadi mashinani.

Seneta Cheruiyot alisema hakuna mzozo katika UDA kwani kinachoendelea ni ukumbatiaji wa kanuni zote za demokrasia katika ulingo wa kisiasa.

“Kongamano la Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) ambalo limeitishwa na chama lina lengo la kuongeza kasi ya uongozi katika uchaguzi wa mashinani unaoendelea na itashughulikia masuala yanayojitokeza. Haihusiani na hali ya kutoelewana katika chama,” Seneta Cheruiyot alisema.

Gavana Mutai, Wabunge – Ngeno, Kemei na Bi Kemei walisema kuna haja ya viongozi kuwaunga mkono Dkt Ruto na Bw Gachagua na kuepuka siasa za migawanyiko.

Walisema wakazi na viongozi kutoka eneo la Bonde la Ufa, ambalo ni ngome ya kisiasa ya Dkt Ruto, wanapaswa kudumisha umoja katika chama cha UDA na utawala wa Kenya Kwanza.

Mzozo katika chama cha UDA

Mzozo katika chama hicho umeshika moto siku chache zilizopita na kuonekana kuwa mbaya zaidi kutokana na vitisho vya Katibu Mkuu Cleophas Malala.

Bw Malala alitangaza atachukua hatua za kinidhamu dhidi ya Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi na mwenzake wa Githunguri Gathoni Wa Muchomba; hii imezidisha mzozo chamani.

Hivi majuzi, usuhuba wa Dkt Ruto na Bw Gachagua umeonekana kudidimia.

Mashambulio ya wazi dhidi ya Naibu Rais kutoka kwa Wabunge yanaonyesha nyufa zimekita mizizi ndani ya chama tawala.

Mbunge wa Githunguri Gathoni Wa Muchomba anaonekana jasiri akikabiliana na Bw Malala punde tu baada yake kumkaripia na wanasiasa wengine mbele ya umma.

“Nadhani kilichokukera ni kwamba kitu tunachodai ni ‘usawa wa rasilimali’ (mtu mmoja kura moja shilingi moja), suala ambalo wewe na wenzako mnatumia kama chambo cha kisiasa. Wakazi wa Mlima Kenya waliamini UDA itawatimizia ahadi hii,” Bi Wamuchomba aliambia Bw Malala.

Kisha akaendelea, “Chama kinaitwa United Democratic Alliance, kumaanisha chama kilianzishwa kwa kanuni za kidemokrasia hasa uhuru na usawa. Una uhuru wa kufanya unachotaka. Nimefurahi umeanza safari ambayo haitakuwa raisi kwako.”

“Ninakotoka (Mlima Kenya)…hatuogopi. Tunakufa huku tukitafuna wembe. Ukigusa kilima, utatikisa mlima,” Bi Wamuchomba alibainisha katika kauli yake.

Gavana wa Bomet Hillary Barchok na Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago wamewaambia viongozi wa Bonde la Ufa kuwa watulivu katika mashambulizi yao dhidi ya Bw Gachagua ambayo yamesababisha nyufa na wasiwasi katika chama.

“Inasikitisha kwamba baadhi ya wanasiasa wachanga na malimbukeni kutoka Bonde la Ufa wamekuwa na mazoea ya kumshambulia Bw Gachagua katika vikao vya umma. Mashambulizi haya yanapaswa kukoma na Naibu Rais apewe heshima anayostahili,” Profesa Barchok alisema.

Bw Mandago alisema, “Lazima tuwe makini katika umoja wa UDA kwani tunazidi kuchekelewa katika ulingo wa kisiasa. Tulianzisha UDA katika mazingira magumu sana na kukifanya kuwa chama imara ambacho Wakenya walikiunga mkono katika uchaguzi mkuu uliopita. Tafadhali tusikivunje sisi wenyewe.”

 “Tunapaswa kuwa waangalifu kama viongozi ili tusisababishe mgawanyiko katika UDA, chama tulichoanzisha na kuwauzia Wakenya waliomchagua Dkt Ruto na Bw Gachagua kuwa Rais na Naibu katika uchaguzi mkuu uliopita. Viongozi wa chama na wanachama wanapaswa kuheshimu Urais kwa kila njia” Bw Ngeno alisema.

“Shambulizi dhidi ya Bw Gachagua ni shambulizo lisilo la moja kwa moja dhidi ya Dkt Ruto, ambalo halipaswi kuruhusiwa kwani huo ni utovu wa nidhamu,” Bw Ngeno alisema akiongeza kuwa lengo lao linafaa kuwa ni kuunganisha wananchi na kutimiza malengo ya serikali ya Kenya Kwanza kabla ya uchaguzi mkuu ujao.