• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
Hongo yatajwa sababu ya madiwani kumwinda Dkt Monda

Hongo yatajwa sababu ya madiwani kumwinda Dkt Monda

NA WYCLIFFE NYABERI

MADIWANI wanaotaka Naibu Gavana wa Kisii Robert Monda ang’atuliwe afisini wametoa sababu tatu zinazotetea Mswada wao  uliowasilishwa bungeni mapema Jumatano.

Diwani wa Ichuni Wycliffe Siocha, aliyeleta hoja hiyo, alidai Dkt Monda alichukua hongo ya Sh800,000 kutoka kwa mkazi mmoja wa Kaunti ya Kisii (Denis Mokaya) ndipo amsaidie kupata kazi katika Kampuni ya Usambazaji Maji na Maji-taka Gusii, GWASCO (Gusii Water and Sanitation Company).

Hata hivyo, mkazi huyo hakupata kazi hiyo kulingana na Bw Siocha.

Kufuatia hongo hiyo, diwani Siocha alisema Dkt Monda alitumia afisi yake vibaya ili kujitajirisha na hivyo akaitaja sababu hiyo kuwa ya pili.

“Kulingana na katiba, kiongozi yeyote anayeshikilia wadhfa serikalini hafai kutumia afisi yake vibaya kujitajirisha. Kwa kuchukua hongo hiyo na baadaye kutishia familia ya mlalamishi aliyekosa nafasi ya ajira ni kutumia vibaya afisi yake,” Bw Siocha alisema.

Diwani huyo pia alidai kwamba Dkt Monda amekuwa akiwatumia vibaya maafisa wa kutekeleza amri za kaunti, almaarufu kama kanjo.

Bw Siocha alidai kuwa Dkt Monda alikuwa amewachukua maafisa watano wa ‘kanjo’ kumtumikia nyumbani kwake katika shamba alilopewa na babake.

Hoja ya mwisho iliyoibuliwa ni kuwa Dkt Monda alijaribu kumhonga Meneja Mkuu wa GWASCO (Lucy Wachira) ili uteuzi wa Meneja wa Mauzo wa kampuni hiyo ufanyike kulingana na mapenzi yake.

Mswada wa Bw Siocha uliungwa mkono na  diwani mteule Callen Magara.

Gavana wa Kisii Simba Arati hajakuwa na uhusiano mzuri na Dkt Monda.

Hii ni kwa sababu mahasimu wake kisiasa akiwemo mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro na Japheth Nyakundi (Kitutu Chache Kaskazini) ni marafiki wakubwa wa Dkt Monda.

Wengine ni Daniel Manduku (Nyaribari Masaba), Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kisii Dorice Aburi na baadhi ya madiwani (MCAs) ambao mnamo Novemba 25, 2023, walikutana na Dkt Monda katika boma lake lililoko kijijini Rigena, eneobunge la Nyaribari Chache. Mkutano huo ulifanyika usiku.

Japo viongozi hao waliwaambia wanahabari kuwa mkutano wao ulikuwa wa kutathmini jinsi ya kufanikisha maendeleo katika kaunti hiyo, ilionekana wazi kwamba viongozi hao walikuwa wakipanga njama kuhusu namna ya kumtenga Gavana Simba Arati dhidi ya viongozi wengine wa kaunti hiyo.

Mkutano huo kwa Dkt Monda ulijiri muda mfupi tu baada ya wanasiasa hao kuhudhuria hafla ya misa katika Kanisa Katoliki la Nyabururu ambapo Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alikuwa mgeni wa heshima.

  • Tags

You can share this post!

Penzi la boi jirani tamu kuliko la mume wangu

Matumaini deni la Kenya la Sh11 trilioni litapungua thamani...

T L