JAMVI: BBI ilivyomlewesha na kumpofusha Raila
Na BENSON MATHEKA
Kabla ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) kutoa ripoti yake ya mwisho iliyozinduliwa katika ukumbi wa Bomas, kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga alikuwa akisema maoni ya kila Mkenya yatashirikishwa kwenye kura ya maamuzi.
Wakati wa kuzinduliwa kwa ripoti hiyo, alisisitiza kuwa mchakato huo ulikuwa wa Wakenya na walio na malalamishi walikuwa na haki ya kuyawasilisha ili kuepusha nchi kugawanyika wakati na baada ya kura ya maamuzi.
Hata hivyo kwa wakati huu, Bw Odinga amebadilisha nia na kupuuza wote wanaopendekeza mswada huo kupigwa msasa akisema hakuna maoni mapya yatakayokubaliwa.
Ingawa alianzisha mchakato huo pamoja na Rais Uhuru Kenyatta, Bw Odinga amekuwa msitari wa mbele kupigia debe mageuzi ya kikatiba huku akiwapuuza wote anaohisi kwamba wanapinga juhudi hizo.
Wadadisi wanasema kwamba kauli yake inamsawiri kama mtu aliyelewa na mchakato huo akitaka upitishwe bila kusikiliza maoni ya watu anaochukulia kuwa mahasimu wake wa kisiasa.
“Bw Odinga amezama katika BBI hivi kwamba imemfanya bubu na kiziwi. Anapuuza chochote kutoka kwa watu anaohisi kwamba wanapinga BBI hata kama wana maoni mazuri ya kuimarisha mchakato huo. Hii ni hatari ambayo athari zake zitamwandama baadaye,” asema mchanganuzi wa siasa Geff Kamwanah.
Bw Odinga amepuuza ushauri wa viongozi wa kidini ambao walipendekeza mswada wa BBI ufanyiwe mageuzi kabla ya kuwasilishwa kwa kura ya maamuzi.
Kulingana na Bw Odinga, viongozi wa kidini walikuwa na wakati wa kuwasilisha maoni yao kwa jopokazi lililokusanya maoni kwa miaka miwili. Kulingana na Bw Kamwanah, kauli ya Bw Odinga imemfanya kutotofautisha kuhusu ukusanyaji wa maoni na mswada ambao utawasilishwa kwa kura ya maamuzi.
“Malalamishi ya sasa sio kuhusu maoni. Kwa hakika, viongozi wa kidini aliopuuza waliwasilisha maoni kwa jopokazi la BBI. Kinachozungumziwa kwa sasa sio ripoti, ni mswada uliotokana na ripoti hiyo na uhalali wa mchakato wa kubadilisha katiba ambao, wataalamu wanahisi kwamba haukuwa wa kisheria,” asema Bw Kamwanah.
Licha ya wataalamu kukosoa mchakato huo na yaliyopendekezwa, Bw Odinga ametia nta kwenye masikio na kusisitiza kuwa ni lazima katiba ibadilishwe. Baadhi ya wataalamu ambao wamekosoa BBI ni Profesa Yash Pal Ghai, PLO Lumumba na Profesa Kivutha Kibwana wanaodai kuwa katiba ya 2010, ambayo Bw Odinga alipigania inafaa kutekelezwa kikamilifu.
“Kuna dharura gani ya kubadilisha katiba,” Profesa Lumumba amenukuliwa akihoji mara kadhaa.
Ingawa wataalamu wanasema kwamba mchakato wa BBI sio wa kisheria kwa kuwa ulianzishwa na kusukumiwa Wakenya na serikali, Bw Odinga amekuwa akisisitiza kuwa yaliyoshirikishwa kwenye mswada huo ni maoni ya Wakenya wengi na waliyopendekeza na makundi kadhaa yakiwemo ya viongozi wa kidini hayangezingatiwa.
Hii ni tofauti na mshirika wake katika BBI Rais Kenyatta ambaye wakati wa kuzindua ukusanyaji wa saini za kuunga mswada huo alifichua kuwa alikutana na makundi ya waliolalamika wakiwemo viongozi wa kidini na kuwasikiliza.
Tumtambue Mungu katika katiba
“Baadhi ya makundi niliyoshauriana nayo kuna jambo moja ambalo viongozi wa kidini waliniambia na nikaona inafaa kwetu kama nchi. Walisema tutambue Mungu katika katiba ambaye amelinda na anaendelea kulinda nchi yetu,” Rais Kenyatta alisema.
Ingawa Bw Odinga amekuwa akimshambulia Naibu Rais William Ruto akidai anataka kupinga mageuzi ya katiba, Rais Kenyatta alikutana naye na baadhi ya masuala aliyotaka yashirikishwe kwenye mswada wa BBI ambayo waziri huyo mkuu wa zamani alikuwa amepinga yalizingatiwa.
Kiongozi huyo wa ODM amekumbatia mchakato huo hivi kwamba amefumbia macho na masikio masuala muhimu kama vile gharama ya kuendesha serikali itakayoongezeka katiba ikifanyiwa mageuzi, gharama ya kuendesha kura ya maamuzi wakati nchi inakabiliwa na hali mbaya ya uchumi na janga la corona.
Wachanganuzi wanasema kwamba amelewa na mchakato huo kiasi cha kukiuka kanuni za kuzuia corona alipoongoza kampeni ya kukusanya saini maeneo tofauti nchini.
Baada ya kuzinduliwa kwa ukusanyaji wa saini za kuunga mchakato huo, Bw Odinga alizuru Mombasa na Murang’a ambako alihutubia mikutano ya halaiki kinyume na kanuni za kuzuia kusambaa kwa corona. Hii ni licha ya viongozi wengine, akiwemo Dkt Ruto kusitisha mikutano ya hadhara baada ya maambukizi ya corona kuongezeka.
Kulingana wadadisi wa siasa, Bw Odinga amepagawishwa na BBI hivi kwamba hajali masuala mengine yanayoathiri nchi.
“Amepagawa kabisa na mchakato huu hata hajali madaktari wanakufa kutokana na corona. Hii ndiyo sababu aliwaambia hawafai kugoma kwa kuwa sio wao pekee wanaouawa na maradhi hayo,” alisema mwanaharakati Lucia Ayiela wa Kongamano la Mageuzi.
Mnamo Jumatatu akiwa Kisumu, Bw Odinga alisema wahudumu wa afya hawafai kugoma wakati nchi inakabiliwa na janga la corona na hali mbaya ya uchumi.
Kauli hiyo ilimsawiri Bw Odinga kama anayetambua BBI kama suala muhimu pekee kwa nchi kwa wakati huu ambayo rasilamali zote zinapaswa kutumiwa kuifanikisha.
Wadadisi wanasema kwamba kinachomfanya Bw Odinga kusukuma BBI ni manufaa anayotarajia kupata binafsi na wandani wake wa kisiasa.
“Bw Odinga anaamini kwamba BBI ndio tiketi ya kumpeleka ikulu kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Hii ndiyo imemfanya kulewa na mchakato huu. Anachojali kwa sasa ni maslahi yake anayoamini ataafikia kupitia mageuzi ya katiba,” asema Kamwanah.