• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
JAMVI: Hofu ya uyatima wa kisiasa inavyogeuka laana Mlimani

JAMVI: Hofu ya uyatima wa kisiasa inavyogeuka laana Mlimani

Na WANDERI KAMAU

MAKABILIANO yaliyotokea katika Kaunti ya Murang’a na kusababisha vifo vya watu wawili Jumapili iliyopita, yameibukia kuwa ‘laana’ kuu inayoliandama eneo la Mlima Kenya, siasa za kumrithi Rais Uhuru Kenyatta zinapoendelea kushika kasi.

Ingawa kambi za ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’ zimekuwa zikielekezeana lawama tangu tukio hilo, wadadisi wanataja uhasama wa kisiasa unaoshuhudiwa katika eneo hilo kama ukosefu wa uongozi thabiti wa kisiasa kama ilivyokuwa katika miaka ya awali.

Baadhi ya viongozi wanaosifiwa kuwa “nguzo ya kisiasa” ukanda huo ni marehemu Njenga Karume, JJ Kamotho, Kenneth Matiba, Johh Michuki, Mzee Jomo Kenyatta, Rais Mstaafu Mwai Kibaki kati ya wengine.

Wadadisi wanasema kuwa kinyume na sasa ambapo kambi hizo mbili pinzani zinawashirikisha viongozi wachanga na malimbukeni kwenye siasa, vigogo hao wa awali kisiasa walizingatia sana maslahi na mustakabali wa eneo hilo.

“Viongozi kama Karume na Michuki walikuwa wenye maono makubwa na hawangesita kamwe kutoa sauti zao ikiwa eneo hilo lingeanza kuyumba kisiasa. Uongozi wao pia ulilijumuisha Baraza la Wazee la Jamii ya Agikuyu (KCE) ambalo pia liliwashirikisha wazee wa hadhi na walioheshimika sana. Kwa mshikamano huo, waliweza kudhibiti usemi na mwelekeo wa siasa Mlimani,” asema Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mwanahistoria na mdadisi wa siasa.

Kwa mujibu wa Prof Macharia Munene, ambaye ni mhadhiri wa somo la Sayansi ya Siasa, ni chini ya uongozi wa vigogo hao ambapo eneo lilibaki thabiti kisiasa, licha ya kuwa kwenye Upinzani kwa karibu muda wote aliotawala marehemu Daniel Moi.

Viongozi wengi walioongoza harakati za kumshinikiza Moi kuleta mfumo wa vyama vingi nchini mnamo 1991 walitoka katika ukanda huo.

“Walipoanza harakati za kumkabili Moi kuruhusu uwepo wa vyama vingi vya kisiasa nchini, ndoto za viongozi kama Kibaki na Matiba zilikuwa kuleta ukombozi wa kisiasa. Waliunganishwa na ndoto hizo, sawa na wafuasi wao, ambapo wengi walitoka katika eneo hilo. Mshikamano huo wa kimawazo na kisiasa ndio ulileta uthabiti mkubwa wa kisiasa Mlimani Kenya,” asema Prof Munene.

Hata hivyo, anataja mazingira ya sasa kuwa tofauti sana, kwani viongozi wengi wa hadhi hiyo hawapo, huku wachache waliobaki wakikosa usemi kwenye siasa za ukanda huo.

KIMYAKIMYA

Kwa mfano, Bw Kibaki amekuwa akiendesha maisha yake kimyakimya, bila kuingilia masuala ya siasa nchini.

Prof Munene anataja pengo hilo la uongozi “kama linalotoa nafasi ya mvurugano wa makundi kama ‘Kieleweke’ na ‘Tangatanga’.”

“Mlima Kenya sasa ni kama uwanja ulio wazi kwa kila mchezaji kuingia na kucheza kila upande anaotaka bila maelekezo yoyote. Inasikitisha kuwa makundi haya hayana msingi wowote kifalsafa, bali lengo lake kuu ni kuwafaidi wanasiasa walioyaanzisha,” asema Prof Munene.

Kundi la ‘Tangatanga’ limekuwa likijisawiri kama “linalomtetea” Naibu Rais William Ruto dhidi ya “kuhangaishwa na serkali” huku likipigia debe azma yake kuwania urais nchini mnamo 2022.

Wale ambao wamegeuka kuwa sauti kuu za kundi hilo ni wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Kimani Ichungw’a (Kikuyu), Rigathi Gachagua (Mathira), Moses Kuria (Gatundu Kusini) na Alice Wahome (Kandara).

Nalo kundi la ‘Kieleweke’ limekuwa likijisawiri kama “mtetezi mkuu” wa Rais Uhuru Kenyatta “dhidi ya mahasimu wake kisiasa ili kumwezesha kutekeleza ajenda yake ya maendeleo.”

Wale ambao wamekuwa wakihusishwa sana na kundi hilo ni wabunge Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), Maina Kamanda (mbunge maalum), Gathoni Wamuchomba (Kiambu), Kanini Keega (Kieni) kati ya wengine.

Wadadisi sasa wanaonya kuwa itabidi Rais Kenyatta achukue udhibiti wa eneo hilo kisiasa, la sivyo huenda migawanyiko ikazidi kushika kasi na kufikia kiwango hatari.

Wanasema kuwa makundi ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’ yanawashirikisha wanasiasa wachanga, ambao wanatumia umaarufu mdogo walipata kujaribu kujijenga.

“Chini ya majibizano na hali iliyoshuhudiwa Jumapili, kuna hatari Mlima Kenya kuwa kama eneo la Magharibi, ambalo halina kiongozi yeyote maalum kisiasa. Hilo limelifanya kuwa ngome ya makabiliano ya kila aina kisiasa,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Hata hivyo, wabunge wanaoegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ wanataja mkasa ulioshuhudiwa Murang’a kama “njama zilizopangwa” ili kumsawiri Dkt Ruto kama kiongozi anayeendesha na kuunga mkono machafuko ya kisiasa.

Kwa mujibu wa Bw Ichung’wa, ambaye ni mshirika wa karibu wa Dkt Ruto, imefikia wakati eneo “lijikomboe kutoka utumwa wa kisiasa wa familia kadhaa tajiri.”

“Inasikitisha asilimia kubwa ya wenyeji Mlimani ni maskini, licha ya eneo hilo kuwatoa marais watatu. Silengi kumkosea heshima wala kumlaumu yeyote, lakini imefikia wakati eneo limuunge mkono kiongozi mwingine tofauti,” asema Bw Ichung’wa.

Hata hivyo, watetezi wa Rais Kenyatta wanasema hakuna pengo lolote la uongozi lililopo kwani bado ndiye msemaji rasmi kisiasa wa eneo hilo.

You can share this post!

Nassor Kharusi: Mazingira ya Zanzibar yalipalilia kipaji...

TAHARIRI: Vutapumzi itumike vilivyo kupunguza ajali