JAMVI: Kauli za Murathe zaacha wengi njia panda
Na BENSON MATHEKA
NAIBU mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe amewakanganya Wakenya kwa kubadilisha msimamo wake kuhusu siasa za urithi wa Rais Uhuru Kenyatta.
Ingawa amekuwa akikariri kwamba Rais Kenyatta hana nia ya kumwachia hatamu za uongozi Naibu Wake William Ruto anayemlaumu kwa kudharau kiongozi wa nchi, Bw Murathe amekuwa akitetereka kuhusu ni nani ambaye anafaa kuongoza nchi mwaka wa 2022.
Mnamo Desemba 2019 wakati kampeni za Mpango wa Maridhiano (BBI) zilikuwa kileleni, Bw Murathe alinukuliwa akisema kwamba Rais Kenyatta hatastaafu siasa, kauli iliyochukuliwa na wandani wa Dkt Ruto kwamba kiongozi wa nchi anaweza kushikilia wadhifa wa juu serikalini Katiba ikibadilishwa.
Wakati huo, duru zilisema kwamba Rais Kenyatta alikuwa akimezea mate kiti cha waziri mkuu mwenye mamlaka.
Mchakato wa maridhiano unaendelea na ni ripoti ya mwisho inayotarajiwa wakati wowote itakayotoa mwelekeo wa iwapo Rais Kenyatta atabaki kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya kwa kuwa serikalini.
Tangu alipoashiria kuwa huenda Rais Kenyatta akaendelea kuwakilisha Mlima Kenya katika siasa za kitaifa baada ya 2022, Bw Murathe amenukuliwa mara kadhaa akitambua wanasiasa anaowekea upatu kumrithi Rais Kenyatta 2022.
“Kauli yake ya hivi punde ilikuwa ya kudai kuwa Waziri wa Kilimo Peter Munya ameiva kuwa msemaji wa Mlima Kenya. Ni kauli iliyotafsiriwa na wengi kwamba kuna minong’ono ya kumfanya gavana huyo wa kwanza wa Kaunti ya Meru kuwa mrithi wa Rais. Hii ilijiri siku chache baada ya Bw Murathe kutoa kauli iliyozua mdahalo mkali mtandaoni akiwataka wakazi wa Mlima Kenya kujiandaa kwa urais wa kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga,” anasema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.
Kabla ya kutoa kauli iliyochukuliwa kama kumtawaza Bw Odinga kuwa chaguo la Rais Kenyatta kuwa mrithi wake 2022, Bw Murathe aliungana na aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth, Bw Odinga na Seneta wa Siaya James Orengo nyumbani kwa Katibu Mkuu wa Muungano wa vyama vya wafanyakazi Francis Atwoli ambapo alisema walijadili siasa miongoni mwa masuala mengine.
Wadadisi walisema kwamba hii iliashiria kuwa Bw Murathe anamuandaa Kenneth au alituma ishara kwamba waziri msaidizi huyo wa wizara ya fedha anaweza kutoshea viatu vya Rais Kenyatta.
“Murathe ni mwanasiasa mwerevu sana. Anajua kupanga na kupangua siasa na analotamka huwa lina lengo fulani. Kila kauli anayotoa inafaa kuchukuliwa kwa uzito unaostahili. Ole wao wanaolichukulia kwa mzaha. Kwa hivyo, anapotambua kiongozi fulani, anamaanisha amekuwa mtiifu kwa rais au amefuata mkondo wa rais. Ukisikia sauti yake kuhusu suala fulani, fuatilia utaona yatakayotokea,” asema mdadisi wa siasa, Bonny Kasuki.
Anasema kwa wakati huu, Bw Odinga anafuata mkondo wa Rais Kenyatta, Bw Kenneth amesema kwamba Mlima Kenya watafuata mwelekeo wa kisiasa ambao eneo hilo litapatiwa na Rais Kenyatta, Munya pia ni waziri mtiifu wa serikali ya Rais Kenyatta.
“Katika siasa, hauaniki mbinu zako sote hadharani. Unacheza na akili za watu na kuacha wapinzani wako wakifaruka huku ukijipanga. Hivi ndivyo Murathe anavyofanya kwa niaba ya Mlima Kenya ikizingatiwa kwamba kipindi cha pili cha utawala cha Rais Kenyatta kinaelekea ukingoni,” asema Bw Kasuki.
Kulingana na Bw Kamwanah, Murathe anacheza kamari ya kisiasa kuhakikisha kuwa serikali ijayo italinda maslahi ya wakazi wa eneo la Mlima Kenya.
“Kwa sasa, muhimu kwa wakazi wa Mlima Kenya ni utawala utakaolinda maslahi yao utakuwa katika BBI ikiwa itafaulu au katika muungano wa kisiasa utakaohusisha viongozi anaotaja miongoni mwa wengine,” asema Bw Kamwanah.
Mdadisi huyo anakumbuka kwamba mnamo 2018, Bw Murathe alifanya mazungumzo na kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi nyumbani kwake Gatanga.
“Wakati huo minong’ono ilikuwa walikuwa wakisuka masuala ya kisiasa. Ingawa Mudavadi anaonekana kufuata mwelekeo tofauti, kumbuka amesema anaunga ajenda za Rais Kenyatta. Murathe pia alikuwa kwenye karamu ya kukaribisha mwaka ya viongozi wa Ukambani nyumbani kwa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ambaye pia anaunga rais. Anafanya hayo yote kwa maslahi ya Mlima Kenya baada ya 2022,” alisema.
Wadadisi wa siasa wanakubaliana kuwa kauli za Bw Murathe sio za kupuuzwa ikizingatiwa ukuruba na utiifu wake kwa Rais Kenyatta kwa miaka mingi.