JAMVI: Makonde ya Joho na Mvurya yaongezeka kura za Msambweni
Na MOHAMED AHMED
ZIKIWA zimesalia siku chache pekee kabla ya uchaguzi mdogo wa Msambweni ufanyike, wawaniaji wa kiti hicho wameendelea kupimana nguvu huku wakiwaacha wengi na wasiwasi wa yule atakayeibuka mshindi.
Kampeni hizo sasa zimewaacha wawaniaji na mahasimu wa karibu Omar Boga wa ODM na Feisal Bader ambaye ni mgombea huru anayeungwa mkono na Naibu Rais William Ruto kutegemea ushawishi wa magavana wawili wa Pwani kukwaruzana.
Gavana wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kwale Salim Mvurya sasa wameonekana kuchukua usukani wa kuendesha kampeni hizo ambazo zimefufua upya uhasama wao wa kisiasa.
Bw Joho anampigia debe Bw Boga naye Bw Mvurya anamuunga mkono Bw Bader. Kuingia kwa magavana hao katika kampeni hizo kumefanya kampeni kupamba moto huku viongozi hao wakitupiana cheche za maneno.
Bw Joho ambaye amekita kambi Msambweni amejitosa katika malumbano na Bw Mvurya ambaye amemuonya Bw Joho kuhusiana na siasa za kujipiga kifua.
Bw Mvurya pia amepinga madai ya Bw Joho kuwa Bw Boga ni mgombea wa serikali ambaye anayeungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta pamoja na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
“Chama cha Rais ni kile cha Jubilee na mimi ni gavana wa Jubilee, kwa hivyo msiambiwe na mtu kuwa kuna mgombeaji wa Rais Msambweni. Msikubali kutekwa na siasa za vyama,” Bw Mvurya amekuwa akimjibu Joho mara kwa mara.
Katika kampeni za Bw Boga, Bw Joho amekuwa akisisitiza kwamba mgombea huyo wa ODM ndiye pendekezo la Rais Kenyatta na Bw Odinga na kuongeza kuwa “Ni kupitia kwake ambapo wakazi wa Msambweni wataweza kupata miradi ya maendeleo kwa urahisi.”
Huku siasa hizo zikiendelea kupamba moto, uchunguzi wa hivi majuzi uliofanywa na shirika la Tifa ulionyesha kuwa Bw Boga ndiye chaguo la wengi iwapo uchaguzi huo ungefanyika wakati wowote sasa.
Katika utafiti huo, Bw Boga angepata asilimia 54 ya kura, huku asilimia 29 wakimpigia Bw Feisal Bader. Wawaniaji wengine wakiwemo Bw Ali Hassan Mwakulonda wa chama cha Peoples Economic Democracy (PED) pia waliorodheshwa kwenye utafiti huo na kuonyesha kuwa angeibuka wa tatu kwa kuzoa asilimia tisa ya kura. Bw Mwarere Wamwachai angeibuka wa nne kwa kupata asilimia mbili ya kura.
Hata hivyo, utafiti uliofanyika kati ya Novemba 29 na Desemba 1 kutoka kwa wakazi 320 ulionyesha kwamba asilimia mbili ya wapigakura hawajui mwaniaji watakayempigia kura. Idadi kama hiyo ilikataa kuelezea mwaniaji watakayempigia kura.
Utafiti huo pia ulionyesha kuwa asilimia 48 ya wenyeji wanaunga mkono ODM huku asilimia 24 wakiunga mkono Chama cha Jubilee (JP).
Asilimia tatu wanaunga mkono chama cha Wiper, huku kiwango kama hicho wakiunga mkono PED. Asilimia nne ilieleza kuunga mkono vyama vingine vya kisiasa.
Asilimia 42 ilitaja manifesto ya Bw Boga kama sababu kuu ya kumfahamu kwa kina, huku asilimia 48 ya wale wanaomfahamu Bw Bader ikitaja utendakazi wake.
Vile vile, ripoti hiyo ilieleza kuwa Bw Boga ndiye anayefahamika zaidi na wapigakura kwa kiwango cha asilimia 43, akifuatwa na Bw Bader kwa asilimia 36.
Bw Bader ndiye aliyesimamia Hazina ya Eneobunge (CDF) wakati marehemu Bw Suleiman Dori alihudumu kama mbunge wa eneo hilo.
Wakati huo huo, asilimia 34 ya wenyeji walisema wanampendelea Bw Boga kutokana na utendakazi wake. Bw Boga alihudumu kama diwani wa wadi ya Bongwe/Gombato kati ya 2013 na 2017.
Hata hivyo, ripoti ilieleza kuwa huenda matokeo ya utafiti huo yakatofautiana na matokeo halisi ya uchaguzi huo uliopangwa kufanyika mnamo Disemba 15.
Aidha, utafiti huo ulionyesha kuwa asilimia 42 ya wale watakaopiga kura walisema watarejelea shughuli zao za kawaida huku asilimia 43 wakisema matokeo hayatawaathiri hata kidogo.
Asilimia saba ilisema kutakuwa na wizi wa kura, asilimia tatu ikaeleza kuhofia kuambukizwa virusi vya corona, nayo asilimia nne ya wenyeji ikaeleza kuhofia ghasia kuzuka.
Kwa sasa itasalia kuangaliwa iwapo utafiti huo utaenda kama ulivyotabiriwa huku wadokezi wa Jamvi wakieleza kuwa kuchacha kwa kampeni huenda kukabadili mambo.
Wachanganuzi wa kisiasa sasa wataangalia namna kampeni hizo zitakavyosaidia wangombeaji hao wanapoomba kura katika siku za mwisho wiki hii.