Je, Ida ndiye mkombozi wa ODM?
CHAMA cha ODM kwa sasa kiko katika kipindi cha misukosuko mikubwa, ambapo kila kikao na mjadala wake umejaa sintofahamu.
Hata kumbukumbu za kihisia za kile ambacho kingekuwa maadhimisho ya miaka 81 ya kuzaliwa kwa Raila Odinga wiki iliyopita hazikufaulu kuziba mipasuko inayotikisa chama hicho.
Kadiri hali hiyo inavyoendelea, Ida Odinga, mama mlezi ambaye kwa muda mrefu amekuwa nguzo tulivu lakini thabiti nyuma ya uongozi wa Raila, sasa amejitokeza hadharani.
Katika pengo lililoachwa na kifo cha Raila, Ida anajitokeza si tu kama mjane mwenye huzuni, bali pia kama nguzo ya maadili na mkakati kwa ODM inayoonekana kuyumba chini ya uongozi wa kaka wa Raila, Dkt Oburu Oginga.
Wasaidizi wake wanasema amelazimika kutoka kivulini ili kuokoa chama dhidi ya hatari ya mgawanyiko.
“Mume wangu aliwaachia chama kilicho imara. Lazima mkilinde na kukidumisha, hata kama si kwa lolote, basi kwa heshima ya kumbukumbu yake,” alinukuliwa akisema kwa mkutano na vigogo wa chama nyumbani kwake wiki iliyopita, kulingana na watu wawili waliokuwapo.
Katika mkutano wa Jumatano katika makazi yake ya Karen, ambapo waombolezaji walivaa jezi maalum za Arsenal kuenzi mapenzi ya Raila kwa soka, sauti ya Ida ilisikika wazi na yenye msimamo. “Baba alikuwa na mapenzi mengine, nayo ni mapenzi kwa ODM,” alisema.
Ida alimkumbuka Raila kama mwanamume wa familia na mwanasiasa, akisisitiza kujitolea kwake kwa familia na chama alichoasisi na kujenga.
Kwa maneno yaliyojaa huzuni lakini pia mamlaka, amekuwa akihimiza umoja ndani ya ODM na kutumia heshima yake kujaribu kutuliza jahazi linalotikiswa na majonzi ya kumpoteza kiongozi wake.
“Ni tamanio langu kwamba tuhifadhi ODM kwa heshima ya Raila kama huduma kwa taifa letu,” alisema huku akiwataka viongozi “kutafakari kwa kina na kwa dhati,” na “kukaa chini, kuzungumza na kutatua tofauti zao.”
Wafuasi kadhaa wamekuwa wakitoa wito mitandaoni wakipendekeza Ida achukue hatamu za uongozi wa ODM, wakimtambua kama nguvu iliyokuwa nyuma ya Raila na mlezi wa mikakati yake kwa miongo mingi.
Hata hivyo, nyuma ya pazia, Ida anakabiliwa na mvutano wa kifamilia, akitofautiana kwa upole na binti yake Winnie Odinga kuhusu mwelekeo wa chama, huku hadharani akijaribu kusukuma ajenda ya maridhiano.
Swali kubwa sasa ni iwapo mama huyu mlezi, akitumia maarifa ya kisiasa ya Raila, anaweza kufufua ndoto ya chama cha chungwa na kuongoza wafuasi wake katika enzi mpya bila kiongozi huyo wa kipekee.
Winnie ni miongoni mwa kizazi cha vijana wakakamavu ndani ya chama, wengi wao wakipinga vikali serikali jumuishi inayoongozwa na Rais William Ruto.
Sambamba na majonzi na matumaini mapya, damu changa imefurika ndani ya ODM, ikileta nguvu inayoweza kuimarisha chama au kukipasua zaidi.
Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ameibuka kama ishara ya msukumo huo wa kizazi kipya. Ijumaa, aliandika mitandaoni: “Tunataka ODM iitishwe Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC). Ni wakati wa kuchukua uongozi wa chama. Baada ya Baba ni Babu. Babu kwa sababu. Bila Babu tabu.”
Kwa upande mwingine, mwanaharakati Kasmuel McOure, aliyepata umaarufu wakati wa maandamano ya kupinga ushuru Juni 2024, anasaka ushawishi akijitangaza kuwa “Kaimu Katibu Mkuu wa ODM” na kudai muda wa Edwin Sifuna umeisha.
Wafuasi wake wanaamini juhudi hizo zinaweza kufufua chama kwa kuvutia vijana waliokata tamaa.
Hata hivyo, nguvu hii ya vijana ina makali makubwa. Wito wa Babu wa kuitisha NDC unaweza kuchochea mapambano makali ya ndani na kuwatenga wazee wa chama, huku ikikumbusha mgawanyiko uliolisambaratisha chama cha FORD cha Jaramogi Oginga Odinga miaka ya 1990.
Takriban miezi mitatu baada ya kifo cha Raila mnamo Oktoba 15, 2025, chama alichokijenga kuwa ngome ya upinzani nchini Kenya bado kinapitia majonzi. ODM inaonekana kupitia hatua zilezile za huzuni—kukataa, hasira, majadiliano, huzuni na hatimaye kukubali hali mpya.
Kadiri Kenya inavyoelekea uchaguzi mkuu wa 2027, ODM iko njia panda. Je, itajipanga upya kuzunguka falsafa ya Raila ya haki ya kijamii, ugatuzi na miungano ya kimkakati, au itapasuka vipandevipande kama FORD?
Hatima ya kura zaidi ya milioni 6.9 alizopata Raila mwaka wa 2022 iko hatarini. Je, zitabaki kuwa nguzo ya ODM au zitasambaratika kwa vyama pinzani?
Katika muktadha huu, kauli za viongozi kama Katibu Mkuu Edwin Sifuna za kutaka mazungumzo na umoja, pamoja na mvutano unaoendelea kuhusu matumizi ya fedha za kampeni za 2022, zinaonyesha vita vya ndani vinavyoamua mustakabali wa ODM.
Kwa sasa, macho yote yako kwa Ida Odinga kuona ikiwa atafanikiwa kuwa sauti ya busara na umoja, huenda akaokoa ODM na kuiandaa kwa mustakabali mpya.
La sivyo, chama hicho kinaweza kuingia katika historia kama vingine vilivyotawaliwa na migawanyiko baada ya kuondoka kwa kiongozi wake mkuu.