• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 6:50 AM
Je, kikao cha 3 cha Limuru kitauunganisha Mlima Kenya?

Je, kikao cha 3 cha Limuru kitauunganisha Mlima Kenya?

NA WANDERI KAMAU

JE, eneo la Mlima Kenya hatimaye litapata sauti moja ya kisiasa?

Hilo ndilo swali ambalo limeibuka, baada ya kubainika kwamba viongozi tofauti wa ukanda huo wanapanga kuandaa Kikao cha Tatu cha Limuru ili kujadili mwelekeo wa kisiasa wa ukanda huo.

Taifa Leo imebaini kuwa juhudi hizo zinaendeshwa na kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua, viongozi wa Chama cha Jubilee (JP) wakiongozwa na Katibu Mkuu Jeremiah Kioni, kati ya wengine.

Kwenye mahojiano, wawili hao walisema kuwa lengo lao ni kuliunganisha eneo hilo bila kujali miegemeo ya kisiasa ya viongozi waliopo.

Ingawa vikao vya hapo awali vimefaulu kuliunganisha eneo hilo kisiasa, wadadisi wanasema kuwa huenda kibarua cha sasa kikakosa kuwa rahisi, ikiwa viongozi wakuu hawatakubali kushusha misimamo yao ya kisiasa.

Hata hivyo, wengine wanasema huenda kikao hicho kikawa hatua ya kwanza ya kuliunganisha eneo hilo kisiasa, hasa baada ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Naibu Rais Rigathi Gachagua kuonekana kushusha misimamo yao mikali ya kisiasa waliyokuwa nayo hapo awali.

Kwenye Kikao cha Kwanza cha Limuru kilichofanyika mnamo 1966, Mzee Jomo Kenyatta aliondoa nafasi ya Makamu wa Rais na kubuni nafasi nane za makamu wa rais wa vyama.

Lengo la kikao hicho lilikuwa kumwondoa uongozini makamu wa kwanza wa rais, Jaramogi Oginga Odinga, aliyekuwa naibu kiongozi wa chama.

Kufuatia kikao hicho, chama kilibuni nafasi za makamu wanane wa kiongozi wa chama—kuyawakilisha maeneo manane nchini.

Maeneo hayo ni Nairobi, Kati, Bonde la Ufa, Pwani, Kaskazini Mashariki, Nyanza na Magharibi.

Kwenye Kikao cha Pili cha Limuru kilichofanyika mnamo 2012, Bw Kenyatta alipata ‘baraka’ za viongozi wa Mlima Kenya kuwania urais.

Lengo la kikao hicho lilikuwa kutafuta mwelekeo wa kisiasa wa Mlima Kenya, ikizingatiwa Rais wa Kenya wakati huo, marehemu Mwai Kibaki, alikuwa akistaafu.

Kikao hicho kilimwidhinisha Bw Kenyatta kuwa kiongozi wa ukanda huo,  na kubuni ushirikiano wa kisiasa na viongozi waliokuwa na maono na malengo sawa ya kisiasa, lengo kuu likiwa kupata ushindi kwenye uchaguzi mkuu wa 2013.

Ikizingatiwa vikao hivyo vimekuwa vikifanyika wakati eneo hilo linalenga kufanya maamuzi muhimu ya kisiasa, wadadisi wanasema kuwa dalili zilizopo zinaonyesha huenda eneo hilo hatimaye likapata muafaka na maelewano ya kisiasa.

“Kile kinaonyesha kwamba kuna uwezekano eneo hilo likapata maelewano ya kisiasa, ni hali ya kushuka kwa misimamo mikali ya ambayo tumekuwa tukishuhudia baina ya Bw Kenyatta na Bw Gachagua,” asema Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

Kulingana naye, hatua ya viongozi hao wawili kushusha misimamo mikali ya kisiasa na hata Bw Kenyatta kusema amekubali wito wa kufanya kikao na viongozi wote wa Mlima Kenya, ni ishara kuna uwezekano kikao hicho kikapata mafanikio.

Hata hivyo, anasema kuwa bado kuna changamoto zilizopo, kwani kuna washirika wa viongozi hao wawili wenye misimamo mikali na wanaopinga juhudi zozote za mapatano baina yao.

“Licha ya miito ya maandalizi ya kongamano hilo, ikumbukwe kwamba bado kuna washirika wa viongozi hao ambao hawangetaka kuona mazungumzo yoyote baina yao. Kuna washirika wenye msimamo kwamba Bw Kenyatta alimhangaisha sana Bw Gachagua kutokana na hatua yake kumuunga mkono Rais William Ruto. Vivyo hivyo, kuna wale wanaoshikilia Bw Gachagua na washirika wake wamemkosea heshima sana Bw Kenyatta. Hivyo, muda ndio utakuwa mwamuzi kuhusu ikiwa kongamano hilo litapata mafanikio,” akasema mdadisi huyo.

  • Tags

You can share this post!

Del Monte yasajili G4S kulinda mananasi kwa mazingira ya...

Rais Ruto apiga makofi badala ya kutikisa mguu

T L