• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Jinsi azma ya Raila AUC inavyozima ndoto za wanasiasa Mlimani – Uchambuzi

Jinsi azma ya Raila AUC inavyozima ndoto za wanasiasa Mlimani – Uchambuzi

NA WANDERI KAMAU

HUENDA wanasiasa ambao wamekuwa wakitumia jina la kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga kujijenga kisiasa katika ukanda wa Mlima Kenya wakakabiliwa na kibarua kigumu, ikiwa kiongozi huyo atateuliwa kuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Kulingana na aliyekuwa Naibu Waziri (CAS) wa Elimu katika serikali ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, Bw Zack Kinuthia, wanasiasa hao watakuwa na mtihani mgumu kujiuza kwa raia kwenye uchaguzi wa 2027, kwani hawatakuwa na lolote la kumwelekeza Bw Odinga.

Kwa muda mrefu, wanasiasa wengi wamekuwa wakimlaumu Bw Odinga kwa kuwa “adui” wa kisiasa wa eneo hilo.

Baadhi ya wanasiasa waliowahi na wanaoendelea kuwa wakosoaji wakubwa wa Bw Odinga ni Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah, wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), na John Njuguna ‘Kawanjiku’ (Kiambaa) kati ya wengine wengi.

Hata hivyo, Bw Kinuthia alisema ikizingatiwa haijulikani kuhusu ikiwa Bw Odinga atakuwa kwenye kinyang’anyiro cha urais au la, basi wanasiasa wengi katika ukanda huo watalazimika kutumia mbinu nyingine  kujifanyia kampeni, kwani hawatakita siasa zao katika kumlaumu na kumkosoa Bw Odinga.

“Ikiwa Bw Odinga hatimaye atafaulu kuchaguliwa kama mwenyekiti wa AUC, wanasiasa wengi katika Mlima Kenya wataachwa mataani. Wengi wataachwa kwenye njiapanda, wakishindwa vile watawaambia wananchi, hasa ikiwa hawatakuwa wametimiza ahadi walizotoa kwao. Utabiri wangu ni kuwa, kutokuwepo kwa Bw Odinga kwenye siasa za Kenya kutakuwa mwisho wa baadhi ya wanasiasa,” akasema Bw Kinuthia.

Hata hivyo, alisema kuwa huo ndio utakuwa mwanzo wa “mapambazuko mapya ya kisiasa katika ukanda huo, kwani wakazi wengi watafunguka macho na kuanza kudadisi utendakazi wa viongozi wao”.

“Kwa wakazi wengi wa Mlima Kenya, huu ndio utakuwa mwanzo wao wa kupumbazwa kwa siasa za chuki isiyokuwepo dhidi ya Bw Odinga. Wengi, bila shaka, wataanza kufunguka macho yao kwa kutathmini utendakazi wa wanasiasa hao,” akasema Bw Kinuthia.

  • Tags

You can share this post!

Watalii wang’ang’ania mfupa wa nyangumi kupiga...

Gachagua @59: Mbele iko sawa?

T L