• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Joho kutumia michezo kuvumisha utalii Mombasa

Joho kutumia michezo kuvumisha utalii Mombasa

Na MISHI GONGO

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imeanzisha mikakati ya kutumia michezo kuvutia watalii.

Gavana Hassan Joho, jana alisema utalii umedorora sana na kuna haja ya wadau kutafuta mbinu mpya za kuvutia wageni.

Akihutubia jana wakati wa kuadhimisha siku ya utalii duniani, Bw Joho alisema wako katika harakati za kuboresha utalii wa michezo ili kuwavutia watu wengi zaidi kutoka mataifa ya kigeni.

“Sekta ya utalii imedorora na kuna haja ya kubuni mbinu mpya za kuwanasa watalii zaidi,” akasema.

Seneta wa Mombasa, Bw Mohammed Faki, alimuomba gavana kutumia uhusiano wake mwema na Rais Uhuru Kenyatta, kumrai ajenge barabara za waendeshaji baiskeli jijini Mombasa.

Alisema japo kaunti inajaribu kusukuma watu zaidi watumie usafiri wa baiskeli ili kulinda mazingira, kaunti hiyo haina barabara muafaka za usafiri huo.

“Tunajua uko karibu na Rais, hivyo tunakuomba umwambie atuletee mpango wa kuboresha barabara kama ule unaoendelea jijini Nairobi,” akasema Bw Faki.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa kisiasa kutoka mji huo pamoja na wadau mbali mbali katika sekta ya utalii na afya.

Kauli yake seneta, iliungwa mkono na mbunge wa Changamwe, Bw Omar Mwinyi, ambaye alihimiza kaunti kutenga pesa katika bajeti yake kununua baiskeli na viatu vya magurudumu ili kuwafaa wanaotaka kushiriki katika mashindano hayo lakini wanakosa vifaa.

Mwaka uliopita, Kaunti ya Mombasa iliandaa mashindano ya baiskeli katika juhudi zake za kupigia debe utumizi wake katika usafiri.

  • Tags

You can share this post!

Mutunga ajiunga na vuguvugu jipya la kisiasa

Kahaba aliyefungwa maisha kwa mauaji ya mwenziwe aachwa huru