• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:32 PM
Kalonzo aamua ‘hakuna kusubiri kipenga mbio za Ikulu’

Kalonzo aamua ‘hakuna kusubiri kipenga mbio za Ikulu’

NA WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka, anaonekana kuanza ‘kujipanga’ mapema kwa kinyang’anyiro cha urais 2027, akisisitiza kuwa anafuata nyayo za Rais William Ruto.

Katika siku za hivi karibuni, Bw Musyoka amekuwa akishinikizwa na washirika wake kuhakikisha kwamba atakuwa debeni kwenye uchaguzi huo, wakiutaja kuwa “nafasi yake kutwaa urais”.

Baadhi ya washirika ambao wamejitokeza wazi na kumshinikiza Bw Musyoka kuanza harakati za kujitayarisha kuwania nafasi hiyo ni Gavana Wavinya Ndeti (Machakos), aliyemwambia mwezi uliopita kuanza kampeni katika sehemu tofauti nchini.

“Enda katika sehemu tofauti nchini kuvumisha azma yako. Tuachie eneo la Ukambani,” akasema Bi Wavinya.

Viongozi wengine ambao wamekuwa wakimpa Bw Musyoka shinikizo kama hizo ni Seneta Enoch Wambua (Kitui), anayeshikilia kuwa “nafasi ya Bw Musyoka kuchukua uongozi wa taifa hili umewadia”.

“Bw Musyoka ndiye kiongozi pekee mwenye uwezo wa kumkabili Rais William Ruto kwenye uchaguzi huru na wenye uwazi,” akasema Bw Wambua.

Kwake binafsi, Bw Musyoka amesema kwamba “ataanza kampeni zake za mapema”.

“Lazima nikiri leo kwamba, kama kuna jambo ambalo nimejifunza kutoka kwa Rais William Ruto, alianza kampeni zake mara tu walipochukua uongozi na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta mnamo 2013. Alianza kampeni zake kama kwamba uchaguzi huo ungefanyika siku iliyofuata,” akasema Bw Musyoka, alipohutubu katik Shule ya Upili ya Miumbuni, Kathiani, Kaunti ya Machakos.

Viongozi wengine ambao wamekuwa wakimshinikiza Bw Musyoka kuanza kampeni zake ni wabunge Jessica Mbalu (Kibwezi Mashariki), Patrick Makau (Mavoko), Gideon Mulyungi (Mwingi ya Kati) na Makali Mulu (Kitui ya Kati).

Katika kile kinaonyesha hatua yake ‘kuzingatia’ wito wa wanasiasa hao, Bw Musyoka ashaanza kuzuru sehemu tofauti nchini, akisisitiza kuwa ndiye kiongozi anayefaa zaidi “kuwakomboa Wakenya kutoka changamoto zinazowaathiri”.

Mnamo Jumapili, Bw Musyoka alizuru katika Kaunti ya Meru, ambapo alitangaza kupata uungwaji mkono wa aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Peter Munya.

“Tutashirikiana na Bw Munya kwenye safari hii,”akasema, alipowahutibia wakazi wa eneo la Muthara, Tigania Mashariki.

Bw Munya, kwa upande wake, alisema kuwa Bw Musyoka ndiye mwanasiasa bora kuchukua uongozi wa nchi 2027, kwani ana tajriba pana ya kisiasa, ikizingatiwa alihudumu katika serikali za marais wastaafu (marehemu) Daniel Moi na Mwai Kibaki, na hata kama Makamu wa Rais.

Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Eugene Wamalwa, pia ametangaza atamuunga mkono Bw Musyoka kuwania nafasi hiyo. Bw Wamalwa ndiye kiongozi wa chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K).

Mnamo Jumatatu, polis walimzuia Bw Musyoka kuhutubia mikutano miwili katika miji ya Chuka na Ndagani katika Kaunti ya Tharaka-Nithi, wakisema kuwa hakuwa na kibali.

Bw Musyoka amesema kuwa hatalegeza Kamba juhudi zake za kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa Wakenya.

  • Tags

You can share this post!

Tuzo ya Safal-Cornell: Kuna haja kwa Wakenya ‘kukutana...

DPP aomba Kang’ethe azuiliwe gerezani kumzuia kutoroka

T L