Kalonzo akaangwa kwa kuchochea ukabila
Na LUCY MKANYIKA
KIONGOZI wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, amekashifiwa vikali kwa matamshi yake kwamba watu kutoka jamii ya Wakamba hawapaswi kuwania ugavana Taita Taveta.
Bw Musyoka alikuwa amesema jamii yake inafaa kuacha nafasi hiyo Wataita na Wataveta.Akihutubu katika miji ya Mwatate na Wundanyi jana, kiongozi huyo alisema watu kutoka Ukambani wanaoishi humo wanapaswa kuwania nafasi za naibu gavana, ubunge, seneta na udiwani.
“Sitamruhusu Mkamba yeyote kuwania ugavana Taita-Taveta. Hilo haliwezekani. Lazima mwonyeshe heshima na shukrani kwa nafasi mlizopewa.
“Hamuwezi kutoka Kitui, Machakos ama Makueni na kutaka kuchukua nafasi za uongozi hapa ilhali mnajua wenyeji ni Wataita na Wataveta,” akasema.
Hata hivyo, kauli yake ilikosolewa vikali na wakili Bernard Mwinzi, ambaye ashatangaza nia ya kuwania ugavana katika kaunti hiyo.Bw Mwinzi aliyataja matamshi ya Bw Musyoka kuwa yenye uchochezi na yasiyo na msingi wowote.
“Matamshi hayo ni tishio kwa umoja wa taifa hili,” akasema Bw Mwinzi.Wakili huyo alisema kuwa wakazi wa kaunti hiyo wana haki ya kumchagua yeyote wanayemtaka kuwa kiongozi wao ifikapo 2022. Alisema kuwa kikatiba, ana haki kuwania kila nafasi aitakayo kokote nchini.
“Wakazi wa kaunti hii wanajua wanachotaka. Si Bw Musyoka aliyeniambia kuwania wadhifa huo. Vivyo hivyo, hataniagiza kutowania. Sijawahi kutafuta ushauri kutoka kwake, na wala hawajawahi kutafuta ushauri wowote kutoka kwangu kuhusu jambo lolote,” akasema.
Alipuuza hisia kwamba kauli ya Bw Musyoka ililenga kuleta mshikamano miongoni mwa wenyeji.