Siasa

Kalonzo, Karua vitani kuhusu kubuniwa kwa ‘Kamwene’

January 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

MIZOZO inayoukumba mrengo wa Azimio la Umoja inaonekana kuendelea kudorora, baada ya kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, kutilia shaka kubuniwa kwa vuguvugu la ‘Kamwene’.

Mnamo Jumanne, Bw Musyoka alilitaja vuguvugu hilo kama “butu kisiasa”, akisema hakuna ufanisi wowote wa kisiasa litakalopata.

Vuguvugu hilo lilibuniwa mwishoni mwa mwaka uliopita na wanasiasa wa Azimio la Umoja kutoka ukanda wa Mlima Kenya, lengo lake likiwa “kuongeza sauti na usemi wa eneo hilo.”

Baadhi ya waanzilishi wake ni Kiongozi wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua, Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee Jeremiah Kioni, aliyekuwa Waziri wa Kilimo Peter Munya, kati ya wanasiasa wengine.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni, Bw Musyoka alilitaja kundi hilo kama “lililojikita kwenye ukabila”.

“Vuguvugu hilo halitaenda mahali, kwani msukumo wake mkuu ni wa kikabila. Sitaki kulizungumzia sana, kwani halitaenda mahali hata kidogo,” akasema Bw Musyoka.

Kiongozi huyo alilitaja kundi hilo kama “tishio kubwa kisiasa kwa yeyote atakayejihusisha nalo”.

“Sitaki kulizungumzia sana kundi hili. Linaashiria ubinafsi wa kisiasa. Ningetaka kuwashauri marafiki wangu kuliacha na kufanya kazi kwa pamoja katika Azimio la Umoja,” akasema.

Hata hivyo, kauli ya Bw Musyoka ilionekana kumkwaza Bi Karua, aliyeeleza “kushangazwa kwake na wasiwasi wa Bw Musyoka kuhusu kuanzishwa kwa Kamwene”.

“Ni nini kinachomhofisha ndugu yangu (Kalonzo) kuhusu Kamwene, ambapo amekuwa akilipaka tope kundi hilo kila mara?” akashangaa Bi Karua, kwenye ujumbe alioandika katika mtandao wa X (zamani Twitter) mnamo Jumatano.

Kutokana na majibizano hayo, wadadisi wanayataja kama ishara za wazi kuhusu mzozo unaoendelea kutokota katika Azimio.

Wanaonya kuwa majibizano baina ya Bw Musyoka na Bi Karua hayafai kuchukuliwa kwa urahisi, ikizingatiwa wawili hao ni vigogo wakuu katika mrengo huo.

“Majibizano hayo ni ujumbe wa mapema kwa uongozi mkuu wa mrengo huo, chini ya Bw Raila Odinga, kudhibiti jahazi. Mustakabali wa mrengo huo unayumba ikiwa migawanyiko iliyopo haitadhibitiwa,” asema Bw James Waithaka, ambaye ni mdadisi wa siasa.