Siasa

Kalonzo: Nimeiva kuongoza Azimio

March 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WYCLIFFE NYABERI

KIONGOZI wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amesema ndiye mgombea bora zaidi anayeweza kuongoza muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya kujaza nafasi ya Raila Odinga anayewania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Makamu huyo wa Rais wa zamani ameongeza kuwa kwa vile yeye ni mwanasiasa mzoefu, ana kila linalohitajika kuwaunganisha Wakenya na viongozi ili kupanga mikakati mipya ya nchi, ambayo itawaepusha wananchi kuumizwa na gharama ya juu ya maisha.

“Hata kama Raila Odinga ataenda Addis Ababa, tutaungana. Chama cha Wiper kitakuwa na nguvu Zaidi, hivyo ninawaomba nyote msajiliwe kuwa wanachama waaminifu,” Bw Kalonzo alisema akiwa Kehancha ambapo alihutubia umati kando ya barabara mnamo Jumatano.

Bw Musyoka alikosoa sana utawala wa Kenya Kwanza na akamlaumu Rais William Ruto kwa kuidhinisha mswada mpya wa nyumba za gharama nafuu kuwa sharia.

Sheria hiyo inarejesha ushuru wa lazima wa asilimia 1.5 ya mapato.

“Tutaendelea kupinga kutozwa ushuru kwa nguvu kwa Wakenya ili kufadhili mradi wa nyumba za gharama nafuu. Hili ndilo litakalowarudisha nyumbani. Wanataka kuharibu nchi yetu, lakini tumesema hapana,” Bw Musyoka aliongeza.

Kiongozi huyo wa Wiper alisema Rais Ruto anafaa kuwa na wasiwasi kwa sababu baadhi ya Wakenya ambao wanatatizwa na gharama ya maisha sasa wanampigia kelele kwenye mikusanyiko ya watu.

“Wanataka kutawala kwa kifua. Wakenya wanapowazomea kama ilivyokuwa Kericho na Bomet, wanaanza kuwatisha,” Bw Musyoka alisema.

Alisema utawala wa Kenya Kwanza umeshindwa kutimiza matarajio ya Wakenya wengi jinsi viongozi wake walivyoahidi wakati wa kampeni.

“Shule zinafungwa wiki ijayo kwa sababu serikali haijatuma pesa. Hii ina maana kwamba watalemewa na madeni ambayo wanadaiwa na wasambazaji. Kila mtu Kenya analia. Hakuna jibu lakini kama Azimio, tutasimama na Wakenya,” akasema.

Alilaani hatua ya serikali ya kuhusisha huduma zake zote za malipo kupitia e-Citizen, akisema mfumo huo utatoa jukwaa kwa watu wachache kujitajirisha.

“Kila siku, mamilioni yanakusanywa kupitia jukwaa hilo lakini hawawezi kuwalipa hata madaktari wanaogoma,” akalalamika.

Kiongozi wa Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa alilaumu utawala wa Kenya Kwanza kwa kusema ‘uongo’ kwamba ndani ya siku mia moja madarakani, watawapunguzia Wakenya mzigo wa gharama ya maisha.

“Waliwaambia kuwa ndani ya kipindi hicho, wataweka pesa mfukoni. Mmeziona? Je, zimewekwa kwenye mifuko ya waendesha bodaboda? Pesa hizo zote zinawafaidi wao tu,” Bw Wamalwa alisema.

Viongozi hao wawili ambao wamekuwa wakizuru sehemu mbalimbali za nchi pamoja huku wakipigania nafasi ya uongozi wa Azimio, watazuru kaunti za Kisii na Nyamira leo Alhamisi kabla ya kukamilisha ziara ya siku tatu ya eneo la Nyanza Kusini mnamo Ijumaa kwa kukutana na viongozi wa Kisii.

[email protected]