• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Kanini Kega: Kuna mkono fiche unaomfadhili Nyoro kumpiga vita Gachagua

Kanini Kega: Kuna mkono fiche unaomfadhili Nyoro kumpiga vita Gachagua

NA WANDERI KAMAU

MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega amedai kwamba kuna mkono fiche unaotumia mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro kumpiga vita kisiasa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Bw Kega alisema kuwa ushujaa wa kisiasa ambao ameonyesha mbunge huyo ni nadra, ikizingatiwa yeye bado ni kijana na anahudumu kwa muhula wa pili.

“Nadhani kwamba lazima kuna watu kutoka nje wanaomsukuma Bw Nyoro kuanzisha vita vya kisiasa baina yake na Bw Gachagua. Hawezi kuwakusanya wabunge wengi hivyo bila ‘baraka’ kutoka kwa watu fulani,” akasema Bw Kega kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni, Alhamisi.

Bw Nyoro amekuwa akiendesha mikakati ya kisiasa akitaka kuwa kiongozi na msemaji wa kisiasa wa ukanda wa Mlima Kenya.

Hata hivyo, Bw Kega alimtahadharisha mbunge huyo, akisema kuwa ni mapema sana kwake kuanza kampeni za urais 2032.

“Ni mapema sana Bw Nyoro kutangaza azma ya kuwania urais. Hatujui hata ikiwa tutakuwa hai 2032. Kama kiongozi, ninamshauri kujihadhari na wabunge anaoandamana nao, wanaosema watamuunga mkono kutimiza azma yake ya urais,” akasema Bw Kega.

Wakati huo huo, kiongozi huyo alilaani hatua ya viongozi wa Kaunti ya Murang’a aliyosema inaleta migawanyiko isiyofaa ya kisiasa katika eneo la Mlima Kenya.

Kulingana na Bw Kega, malalamishi ya viongozi hao kwamba kaunti hiyo haijamtoa Rais, Makamu wa Rais au Naibu Rais hapo awali ni ubinafsi wa kisiasa, kwani kuna kaunti nyingi ambazo pia hazijawatoa viongozi kama hao.

“Kisingizio kwamba Kaunti ya Murang’a haijawatoa viongozi wakubwa wa kisiasa ni kisingizio kisicho na umuhimu wowote. Ikumbukwe kwamba kuna kaunti nyingi ambazo hazijawatoa Rais, Makamu wa Rais au Naibu Rais kama vile Nyandarua, Kirinyaga, Meru kati ya nyingine. Hivyo wanafaa kungoja muda wao kufika,” akasema Bw Kega.

  • Tags

You can share this post!

Bobi Wine awekwa ‘chini ya kizuizi’ nyumbani

Kilio kijijini Karibaribi wezi wakilenga wenye maduka,...

T L