Siasa

Kingi aahidi kuadhibu waliomumunya mamilioni ya corona

August 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na ALEX AMANI

GAVANA wa Kaunti ya Kilifi, Bw Amason Kingi, amesema serikali yake itashirikiana kikamilifu na asasi za kuchunguza ufisadi kukabiliana na janga hilo.

Alisema hayo wakati baadhi ya viongozi na mashirika ya kijamii katika eneo hilo wanakashifu utawala wake kwa madai ya kufuja Sh220 milioni zilizotengewa kampeni ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Akizungumza na wanahabari mjini Malindi jana, Bw Kingi alisema serikali yake haitamtetea afisa yeyote atakayepatikana amefuja fedha za umma.

Aliwahimiza wakazi wa kaunti hiyo kuhakikisha wanakagua ripoti kuhusu matumizi ya pesa za janga la corona itakapowasilishwa tena bungeni Jumatatu.

Bw Kingi alisisitiza kuwa, ripoti hiyo inalenga kuweka wazi jinsi pesa hizo zilitumika kuwahudumia waathiriwa wa janga hilo.

“Serikali yangu itashirikisha vitengo vyote katika kuimarisha vita hivi ili kurejesha fedha zilizofujwa. Tuko imara na tunaendeleza vita dhidi ya ufisadi kikamilifu,’ alisema Bw Kingi.

Awali, kamati ya bunge la kaunti ya kukagua utumizi wa fedha za maendeleo iliahirisha mkutano wa kuwahoji mawaziri watatu, Samuel Nzai (Fedha), Gabriel Katana (Ugatuzi) na Charles Dadu (Afya) baada ya kukosa kuridhishwa na ripoti waliyokuwa wameiwasilisha mbele ya kamati hiyo.

Walishtuka kugundua kwamba, Sh10 milioni zilitumiwa kununua sabuni za kipande, na kuagiza ripoti mpya iwasilishwe ili ifafanue jinsi fedha zote za kupambana na janga la corona zilivyotumiwa.

‘Nataka kuwahakikishia kwamba, afisa yeyote atakayehusishwa na kashfa za ufisadi atakabiliwa na mkono wa sheria,’ akasema Bw Kingi.