• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Kuhusishwa na njama kumuua Ruto kulinishtua – Sicily Kariuki

Kuhusishwa na njama kumuua Ruto kulinishtua – Sicily Kariuki

NA WANDERI KAMAU

WAZIRI wa zamani, Bi Sicily Kariuki, ameeleza jinsi alivyoshangazwa na madai kwamba alishiriki kwenye mkutano wa kupanga njama za kumuua Rais William Ruto mnamo 2019, wakati huo akiwa Naibu Rais.

Mkutano huo wa faragha ulidaiwa kufanywa na mawaziri kadhaa, katika hoteli ya La Mada jijini Nairobi.

Kwenye wasifu wake mpya ‘Breaking the Illusions’ (Kuvunja Dhana), Bi Kariuki anasema kuwa madai hayo yalitokana na mivutano ya kisiasa iliyokuwa ikiendelea baina ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto.

Ilidaiwa Bi Kariuki alikutana na mawaziri wengine wawili kupanga njama hizo.

Bi Kariuki ambaye alikuwa waziri wa Maji na pia Afya ya Umma, anasema kuwa alishangazwa sana na simu kutoka kwa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kwamba alifaa kufika katika makao makuu yake, yaliyo katika Barabara ya Kiambu, Nairobi, kuandikisha taarifa kuhusiana na madai hayo.

“Hayo ndiyo madai mabaya sana ambayo mtu anaweza kuhusishwa nayo!” anaeleza kwenye kitabu hicho.

Bi Kariuki anasema kuwa kufikia sasa, bado huwa anashangazwa na madai hayo.

“Kufikia sasa, sijui ukweli kuhusu jambo hilo. Sijawahi kulijadili na Bw Kenyatta au Dkt Ruto. Kile ninajua ni kwamba nilikuwa mwathiriwa wa mahusiano ya kisiasa yaliyoharibika baina ya wawili hao. Ninajua kuna wakati siasa zinaweza kugeuka na kuchukua mkondo mbaya sana na kuwapaka tope watu wasio na hatia yoyote,” anaeleza.

Anaeleza kuwa alifika katika makao ya DCI pamoja na mawaziri hao, lakini akakataa kuandikisha taarifa, kwani hakuna malalamishi rasmi yaliyokuwa yamewasilishwa dhidi yao.

“Malalamishi pekee yaliyokuwepo ni barua iliyokuwa ikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Tuliwashinikiza makachero kutueleza uhalali wa barua hiyo ndipo tuandikishe taarifa,” akaeleza.

Akaongeza: “Makachero hao walituambia kwamba Naibu Rais [Dkt Ruto] alikuwa amepiga simu katika idara hiyo kueleza wasiwasi wake. Walisema hilo ndilo lililowafanya kutuita kuandikisha taarifa hiyo.”

Kitabu hicho kilizinduliwa Ijumaa, jijini Nairobi.

Kimeandikwa na mhariri wa zamani wa gazeti la Daily Nation, Dkt Liz Wanjohi-Gitonga, aliye pia mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Riara.

  • Tags

You can share this post!

Bungei akataa kuzungumzia tukio la mshukiwa wa mauaji...

Tanzia: Mwanasiasa mkongwe Edward Lowassa aaga dunia

T L