Siasa

Kuna mtu ataumia

January 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA WYCLIFFE NYABERI

UHASAMA wa kisiasa baina ya Gavana wa Kisii Simba Arati na Kiranja wa Wengi bungeni Silvanus Osoro, unaozidi kutokota kila kukicha, sasa umefikia viwango vya kutisha huku chama cha ODM kikidai kuwa maisha ya gavana huyo yako hatarini.

Aidha, ubabe huo umeanza kuvutia hisia za Wakenya katika ngazi ya kitaifa huku wadadisi wa siasa wakionya kuwa mfarakano baina ya wawili hao unachochewa na ari ya kila mmoja kutaka kutawazwa msemaji wa jamii ya Abagusii.

Jumatatu wiki hii, katika eneobunge analowakilisha Bw Osoro (Mugirango Kusini), watu wanne walipata majeraha mabaya ya risasi pale waliposhambuliwa na kundi linaloaminika kuwa la mbunge huyo.

Japo Bw Osoro alikanusha madai hayo, ni dhahiri kuwa amekuwa akipimana nguvu na Bw Arati, hata kabla gavana huyo kuhamisha ngome yake ya kisiasa kutoka jijini Nairobi, alikokuwa mbunge wa Dagoretti Kaskazini, hadi Kisii.

Mwanzo, wawili hao walifarakana mnamo Februari 1, 2021, walipolimana makonde mbele ya Rais William Ruto (akiwa naibu rais) na kinara wa ODM Raila Odinga wakati wa mazishi ya aliyekuwa naibu gavana wa Kisii, Joash Maangi katika kijiji cha Riagongera, Bomachoge Chache.

Chanzo cha ngumi hizo zilizotatiza mazishi hayo kwa muda, ni maongezi ya Bw Arati alipomtaka Rais Ruto kuomba jamii ya Abagusii msamaha kutokana na ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007, ambapo watu wengi wa jamii ya Abagusii, waliokuwa wakiishi katika Bonde la Ufa, waliuawa kulingana na Bw Arati.

Matamshi hayo hayakumkalia vyema Bw Osoro aliyesimama kutoka kwenye kiti chake na kuelekea jukwaani alikokuwa akihutubu Bw Arati na kizaazaa cha kuvutana mashati na tai kuzuka.

Bw Osoro ni mfuasi sugu wa Rais Ruto hali Bw Arati ni mwandani wa kinara wa upinzani, Bw Odinga, hivyo basi kupigana kwao kulifasiriwa na baadhi ya watu kuwa tukio la kuwafurahisha vinara hao.

Baada ya uchaguzi mkuu wa 2022, Arati alichaguliwa gavana naye Osoro akarejea kwa mara ya pili kama mbunge wa Mugirango Kusini.

Kwa kuwa Bw Osoro alisimama kidete na Rais Ruto hadi akaingia Ikulu, alizawidiwa kiti cha Kiranja wa Wengi na tangu apokee wadhfa huo, amekuwa akimhangaisha Gavana Arati kila mara anapojaribu kutekeleza wajibu wake kama mkuu wa kaunti.

Lakini Bw Arati naye hajawa rahisi hivyo kusukumwa ukutani. Amekuwa akisema hatayumbishwa na njama zozote za kumhujumu.

Wahudumu wa afya wavamiwa

Mnamo Aprili 2023, baadhi ya wahudumu wa afya katika hospitali ya Nduru, inayopatikana eneobunge la Osoro, walivamiwa na kujeruhiwa na wahuni waliokuwa wakipinga kuhamishwa kwa vifaa fulani vya matibabu. Gavana Arati alimhusisha Osoro na fujo hizo na kusema kuwa wahuni hao walitumwa na mbunge huyo.

Mwishoni mwa Oktoba 2023, afisi za muda za Gavana Arati zilizoko katika uwanja wa michezo wa Gusii zilizingirwa na maafisa wa GSU.

Japo GSU hao walidai walikuja “kupumzika” nje ya afisi hizo walipoulizwa sababu za kuja kwao, Gavana alisema kuwa baadhi ya adui zake kisiasa walitaka kumwingiza baridi kwa kumtumia kikosi hicho kutokana na juhudi zake za kuunganisha wahudumu wa bodaboda mjini Kisii.

GSU hao walipotua Kisii, Osoro alinukuliwa akisema kikosi hicho kitazidi kutumwa Kisii kutuliza hali ya usalama aliyosema ilikuwa imeanza kudorora.

Katika juhudi za hivi karibuni, Bw Osoro pia ameripotiwa kujaribu kumtenganisha Gavana na naibu wake Dkt Robert Monda. Mwishoni mwa mwaka 2023, aliongoza wabunge Japheth Nyakundi (Kitutu Chache Kaskazini), Daniel Manduku (Nyaribari Masaba), Richard Onyomnka (seneta) na Dorice Aburi (mwakilishi wa kike) katika mkutano wa faragha nyumbani kwa Dkt Monda.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Javas Bigambo, sarakasi baina ya wawili hao ni kutokana na ari ya kila mmoja kujaribu kurithi ubabe wa siasa katika jamii ya Abagusii.

“Viongozi hao ni wachanga na hawajaachana sana kiumri. Ikumbukwe kuwa katika uchaguzi wa 2022, jamii ya Abagusii iliwakataa viongozi wakongwe kama vile Prof Ongeri na Dkt Chris Obure. Hawa ndio waliokuwa wakiipa jamii mwelekeo na kwa kuwa hawako, kila mtu anajaribu kujiweka mbele kutwaa uongozi hao,” Bw Bigambo aliambia Taifa Leo.

Hata hivyo, mtaalamu mwingine Dismus Mokua alitoa kauli kinzani na ya Bw Bigambo. Bw Mokua alihoji kuwa enzi za Abagusii kujipanga nyuma ya mwanasiasa fulani kama msemaji wao ziliisha na utawala wa aliyekuwa mbunge wa Nyaribari Chache marehemu Simeon Nyachae.

“Enzi za usemaji Kisii zimepita. Hata hivyo Wakisii wanafaa kuungana nyuma ya mawazo ambayo yanalingana na maslahi ya kijamii na kiuchumi kwao,” Bw Mokua alisema.

Kufuatia vurugu za hivi majuzi za eneo la Mugirango, chama cha ODM kikiongozwa na Katibu Mkuu wake Edwin Sifuna kilimlimbikizia lawama Osoro na kudai mbunge huyo alikuwa amemea “kiburi” kutokana na wadhfa wake wa Kiranja Bungeni na kuongeza kuwa ipo njama ya kumuua Gavana Arati.

Chama cha ODM kinaelezea hofu yake kuhusu maisha na usalama wa Naibu wake wa Kitaifa na Gavana wa Kisii, Simba Arati kutokana na mashambulizi ya kila mara yanayotekelezwa na watu wanaojulikana.”