Kura za damu, uharibifu wa mali na vilio maswali yakizuka kuhusu utayarifu 2027
UCHAGUZI mdogo uliofanyika jana katika maeneo kadhaa ya uwakilishi ulikumbwa na ghasia na uharibifu wa mali katika baadhi ya maeneo huku maswali yakizuka kuhusu utayarifu wa Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Mbunge wa Homa Bay Mjini, Peter Kaluma, alikuwa miongoni mwa waliovamiwa na kujeruhiwa baada ya vijana wenye silaha kuteka maeneo ya Kasipul wakati wa uchaguzi huo mdogo.
Mbunge huyo alipata jeraha kichwani baada ya kupigwa na kitu butu katika Shule ya Msingi ya Agoro Sare, West Kamagak.
Mlinzi wake pia alidai kupoteza bunduki wakati genge la vijana walipowavamia na kuwataka waondoke kituoni.
Hali ya taharuki ilitanda shuleni humo huku makundi hasimu yakitishiana.
Bw Kaluma alikuwa amekita kambi katika kituo hicho akisubiri mgombeaji wa ODM, Boyd Were afike apige kura.
Lakini magari yaliyowasili hayakuwa ya msafara wa Bw Were bali ya mgombeaji huru, Philip Aroko, aliyekuwa tayari amepiga kura katika kituo cha Kachieng.
Kwa muda mfupi wanasiasa hao wawili walikumbatiana kwa furaha, lakini vijana walimtaka mbunge huyo aondoke, baadhi wakimlaumu kwa kununua kura. Hatimaye polisi waliwalazimisha kuondoka kituoni.
“Ninawajua waliotushambulia. Ni genge lililokodiwa kutoka Kibra, Mathare na Ruaraka,” alidai Bw Kaluma.
Polisi wa Homa Bay walisema wanawasaka washukiwa waliomshambulia mbunge huyo na kutoroka na silaha.
Baadaye polisi walinasa magari zaidi ya saba yaliyotumiwa kusafirisha wahuni.
Ghasia pia ziliripotiwa Malava na Lugari. Magari kadhaa, yakiwemo ya mgombeaji wa DAP-K, Seth Panyako, yaliharibiwa na hoteli yake kuvamiwa na watu waliojihami usiku wa Jumatano.
Gari aina ya Toyota Prado linalodaiwa kumilikiwa na mwanasiasa wa upinzani pia lilichomwa moto.
Dereva wa Panyako naye alipata majeraha na kukimbizwa hospitalini.
Bw Seth Panyako, alibubujikwa na machozi kutokana na kile alichotaja kuwa vitisho dhidi ya maisha yake, kuvamiwa na kuharibiwa kwa hoteli yake kwa hali aliyodai kuwa njama ya kuingilia uchaguzi.
Akiongea jana asubuhi akiwa na kiongozi wa DAP–K, Eugene Wamalwa, Panyako alidai maafisa wa usalama walishirikiana na wahalifu kumlenga yeye na mkewe.
“Nilipata taarifa kuwa hoteli yetu ingevamiwa, sikujua ilikuwa kweli hadi walipofika. Serikali kupitia watu fulani ilipewa maagizo kuniua. Hakuna njia nyingine ya kumfanya mgombeaji wao ashinde,” alidai huku akilia.
Alisema hoteli yake ya Downhill Hotel, ilivamiwa na watu aliowaita wahalifu, wakilenga chumba chake, magari yake na ukumbi aliotaka kutumia kama kituo chake cha kujumuisha matokeo.
Katika eneobunge la Mbeere North, kiongozi wa Chama Cha Kazi (CCK), Moses Kuria, alidai kuwa maajenti walivamiwa wakielekea vituoni mapema asubuhi.
Visa vya vurugu viliripotiwa Mbeere North ingawa upigaji kura uliendelea vizuri katika vituo vingi vya kupigia kura.
Katika kituo cha Mathai katika wadi ya Nthawa, mwanaume aliyedaiwa kugawa fedha kwa baadhi ya wapigakura alikamatwa na wananchi, lakini hali ya utulivu ilirejea haraka.
Nyamira, makundi ya vijana wenye mapanga na mishale yalikita kambi katika vituo vya Nyansiongo, Ekerenyo na Nyamaiya, yakitishia wapigakura.
Vijana hao walidaiwa kuongozwa na mbunge mwenye ushawishi kutoka Kisii anayehusishwa na serikali ya Kenya Kwanza.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi waliwazidi nguvu na kuwafukuza. Barabara ya Kisii–Sotik ilifungwa kwa muda ili kuwazuia wasiende vituo vingine.
Katika eneo la Ekerenyo, hali ilikuwa tete baada ya wafuasi wa Mbunge wa North Mugirango, Joash Nyamoko na mwenzake wa Kitutu Chache Kusini, Anthony Kibagendi, kukabiliana wakilaumiana kwa kuhonga wapigakura.
Gari lililobeba marungu lilikamatwa katika Kituo cha Polisi cha Okinge.
Kinyume na maeneo mengine, Ugunja ilikuwa tulivu bila vurugu kubwa lakini wapigakura walikuwa wachache vituoni.
Shule ya Msingi ya Ugunja Township, mojawapo ya vituo vilivyo na wapigakura wengi, ilipokea idadi ndogo sana ya wapiga kura.
Katika wadi ya Mumbuni North, Kaunti ya Machakos, aliyekuwa diwani (MCA) Paul Museku alishambuliwa baada ya kufika kituo cha kupigia kura.
Watu wanaodaiwa kuwa wakazi wa eneo hilo walimvamia mara moja, wakimlaumu kwa kujaribu kuhonga wapiga kura.
Tukio hilo lilitokea alipokuwa akielekea katika kituo cha kupigia kura cha Mung’ala. Polisi waliingilia kati na kumuokoa Museku.
Ripoti za Shaban Makokha, George Odiwuor, Kassim Adinasi, Wycliffe Nyaberi, Ruth Mbula na Pius Maundu