Malala, Linturi, Mwathi miongoni mwa watakaomsaidia Riggy G kusikiza ‘ground’
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa United Democratic Alliance (UDA) Cleophas Malala na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi ni miongoni mwa wale waliotajwa kama viongozi wapya chama cha Democracy for Citizen Party (DCP) chake aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Akisoma majina ya viongozi wa muda wa chama hicho Alhamisi jijini Nairobi, Bw Gachagua alisema Bw Malala ndiye atahudumu kama naibu kiongozi wa chama hicho huku Bw Linturi akihudumu kama Katibu Mratibu.
Bw Linturi, ambaye aliwania ugavana wa Meru 2022 kwa tiketi ya UDA, alijiuzulu rasmi kutoka chama hicho Jumatano wiki hii.
Wadhifa wa Mwenyekiti wa Kitaifa ulimwendea Davidi Mingati Parseina kutoka Kajiado huku aliyekuwa Mbunge wa Limuru Peter Mwathi alitajwa kama naibu wake atakayehusika mikakati.
Katibu Mkuu ni Hezron Obaga kutoka kaunti ya Kisii huku naibu wake akiwa mwanasiasa wa Narok Kaskazini Martin Ole Kamwaro.
Aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Laikipia Catherine Waruguru alitajwa kama Kiongozi wa Kitaifa wa akina Mama huku aliyekuwa Mbunge wa Starehe Maina Kamanda aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa jopo la watu mashuhuri.
Naye mweka hazina wa chama hicho ni Annah Kavuu Mutua kutoka Machakos.
“Majina ya viongozi hao wa muda wa chama chetu cha Democracy for Citizen Party tayari yamewasilishwa kwa Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa,” Bw Gachagua akasema.
Hata hivyo, wanasiasa waliochaguliwa na ambao ni wandani wa Bw Gachagua hawakutunukiwa wadhifa wowote katika chama hicho kipya, japo walihudhuria shughuli hiyo katika mtaa wa Lavington.
Viongozi hao ni pamoja na; maseneta John Methu (Nyandarua, Seki Lenku Ole Kanar (Kajiado), Karungo Thang’wah (Kiambu), Joe Nyutu (Murang’a) na James Murango wa Kirinyaga.
Wengine ni wabunge, James Gakuya (Embakasi Kaskazini), Benjamin Gathiru almaarufu Meja Donkk (Embakasi ya Kati), Jane Kihara (Naivasha), Onesmus Ngogoyo (Kajiado Kaskazini), miongoni mwa wengine.
Bw Gachagua analenga kukitumia chama cha DCP kulemaza kabisa ushawishi wa UDA katika eneo la Mlima Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Aidha, Mbunge huyo wa zamani wa Mathira anapania kukitumia chama hicho kuunda muungano mpya wa kisiasa na vyama vingine vya upinzani kwa nia ya kumwondoa mamlaka Rais William Ruto.
Rangi za chama cha DCP ni: kijani, kahawia na nyeusi huku nembo yake ikiwa mkono unaoshika sikio, kuashiria kusikiza kwa makini kile wananchi wanasema.
Aidha, kauli mbiu cha chama hicho, kilichosajiliwa rasmi mnamo Februari 3, 2025 ni “Sikiza Wakenya” au (Sikiza Ground).
Bw Gachagua anatarajiwa kukivumisha chama hicho kabla ya kubuni muungano na viongozi wa upinzani kama vike kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa (DAP-K), Martha Karua (People Liberation Party-PLP), aliyekuwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’I, miongoni mwa wengine.