Siasa

Maraga: Naweza kuungana na kina Kalonzo lakini kwa Ruto siendi hata kwa dawa

Na BENSON MATHEKA November 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JAJI Mkuu mstaafu, David Maraga, ametaja masharti ya kuungana na vinara wengine wa upinzani akiwemo aliyekuwa waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i kuelekea uchaguzi wa 2027 lakini akapuuza kabisa uwezekano wa kuungana na Rais William Ruto.

Akizungumza katika mahojiano kwenye Obinna Show ya Jumatatu, Novemba 24, 2025, Maraga, anayelenga urais, alitetea uamuzi wake wa kugombea akisema umetokana na msukumo wa vijana waliomiminika barabarani wakati wa maandamano ya kizazi cha Gen Z wakipinga Mswada wa Fedha wa 2024.

Alisema kuwa iwapo, Fred Matiang’i wanayetoka eneo moja anataka kushirikiana naye, basi ni lazima kwanza akubali masharti ya msingi kabisa kwa kuonyesha maono sawa naye kuhusu taifa, ikiwemo kutetea utawala wa sheria na kupambana na ufisadi.

Aliongeza kuwa endapo Matiang’i yuko tayari kuunga mkono maadili hayo, yuko tayari kuketi naye ili kushirikiana kuelekea 2027.

“Akija na akumbatie maono yangu, tutafanya kazi pamoja,” alisema.

Aidha, alisisitiza kuwa hawezi kuachia mtu mwingine azima yake, akisema yeyote anayetaka kufanya kazi naye lazima amkubali kama mgombeaji mkuu na kumuunga mkono.

Kuhusu uwezekano wa kufanya kazi na kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, Maraga alimsifu makamu wa rais wa zamani akisema ni mtu mwema na kufichua kuwa walikuwa darasa moja wakisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Alisema hana tatizo kushirikiana na Kalonzo kwa kuwa ni rafiki yake wa muda mrefu.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa kama ilivyo kwa Matiang’i, Kalonzo lazima pia akubaliane na maono yake kwa taifa kabla ya kushirikiana naye. Bw Maraga alisisitiza kwamba masharti yanawahusu pia wanasiasa wengine wanaolenga urais.

Maraga alikataa vikali uwezekano wa kushirikiana na Rais William Ruto, akisema maadili yao hayalingani. Alikanusha kabisa wazo la kuunda muungano wa kisiasa na Rais Ruto, akisema tofauti zao ni kama “mchana na usiku,” na anayesimamia serikali inayokumbatia ufisadi.

Alisema hawezi kufanya kazi na mtu “anayewaamuru watu wapigwe risasi miguuni,” akisisitiza kuwa njia zao haziwezi kukutana.

Jaji Mkuu huyo wa zamani pia amefichua kuwa maandamano ya Gen Z ya mwaka 2024 yalikuwa chanzo kikuu cha kumsukuma agombee urais akisema alichoshuhudia wakati wa maandamano hayo kilimshtua.

“Sikuwa nikitamani kuwa mwanasiasa. Hatuwezi sote kuwa wanasiasa; watu wengine lazima wafanye mambo mengine. Lakini kile nilichoona mwaka jana kilinishangaza, vijana kupigwa risasi kama panya. Sikuamini kuwa kama nchi tunaweza kuruhusu hilo,” alisema.

Alisema maandamano hayo yalitokana na malalamishi kuhusu Mswada wa Fedha na  badala ya kuzungumza na vijana, serikali ilijibu kwa nguvu kupita kiasi.

“Kisha baada ya muda mfupi unaagiza wapigwe risasi miguuni. Nikajiuliza ‘Tuko Kenya kweli? Tuko nchi gani?’ Sijawahi kusikia mtu yeyote, hata asiye rais, akisema jambo kama hilo. Nikasema, ‘Hili si sahihi’,” aliongeza.

Maraga alisema alishauriana na marafiki waliomhimiza kuingia kwenye uongozi.

“Waliniambia, ‘Maraga, njoo ugombee.’ Wanajua mimi ni mtu thabiti. Nimekuwa nikisema mara nyingi kwamba tuna mojawapo ya katiba bora duniani; tatizo ni utekelezaji wake,” alisema.

Alithibitisha kuwa aliitikia mwito wa vijana wa Kenya kugombea urais 2027. Alisema vijana kutoka maeneo mbalimbali wametambua uongozi wake na rekodi yake nzuri ya utumishi, na wamemsukuma kuingia rasmi kwenye siasa.