Mbunge amtaka Gachagua kujiuzulu
NA JESSE CHENGE
MAMBO yanaendelea kuchemka katika ulingo wa kisiasa huku Mbunge wa Webuye Mashariki Bw Martin Wanyonyi akimtaka Naibu Rais Rigathi Gachagua kufanya uamuzi wa ama kumuunga mkono kikamilifu Rais William Ruto au kujiuzulu wadhifa wake.
Bw Wanyonyi alidai Bw Gachagua hujisawiri kama kiongozi mwenye nia tu ya kuongoza eneo la Mlima Kenya.
Aidha Bw Wanyonyi alisema Katiba ya mwaka 2010 inaruhusu wabunge kuchukua hatua iwapo Naibu Rais ataonekana kuwa ameshindwa kuzingatia sheria na amelemewa na majukumu yake.
Akihutubia wanahabari katika mazishi ya Mzee Julius Opicho katika eneo la Magemo, kata ya Mihuu eneo la Webuye, Bw Wanyonyi alisema mkwamo wa kisiasa unaoshuhudiwa ukiendelea, wabunge hawatakuwa na budi ila kuwasilisha hoja Bungeni kushughulikia mgogoro huo.
“Iwapo Naibu Rais ataendelea na matendo na kauli hizo zake za kukanganya, sisi wabunge hatutakuwa na budi ila kuwasilisha hoja Bungeni,” akasema Bw Wanyonyi.
Mnamo Jumapili Rais William Ruto aliwahimiza viongozi wakiweni wabunge kuendelea kushiriki katika majukumu yao ya kisheria na kuwatumikia wapigakura na raia kwa ujumla huku wakikukuza umoja na mshikamano wa kitaifa.
Kwenye ibada katika Uwanja wa Amutala Kimilili, Kaunti ya Bungoma, Rais Ruto alisisitiza majukumu matatu ya wabunge, akisema ni uwakilishi, kutunga sheria, na uangalizi.
Alisisitiza umuhimu wa Wabunge kuelewa nchi ili kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Ninafurahi kuwa viongozi wengi kutoka sehemu mbalimbali za nchi wamehudhuria ibada hii. Hii ni sehemu ya juhudi zetu za kuleta umoja,” alisema Rais Ruto.
Dkt Ruto aliwaonya viongozi dhidi ya siasa za uchochezi na kuwataka Wakenya kukataa viongozi wanaopandikiza mgawanyiko na chuki.
“Tuna mambo mengi ya kufanya kama viongozi. Tujielekeze katika kuiendeleza nchi na sio kwa kugawa nchi kwa misingi ya kikabila,” alisema.