• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 6:55 PM
Mjane wa Murunga kuwania ubunge Matungu

Mjane wa Murunga kuwania ubunge Matungu

Na Shaban Makokha

MJANE wa aliyekuwa mbunge wa Matungu Justus Murunga, Bi Christabel Murunga, ni miongoni mwa wawaniaji wanane ambao wameidhinishwa kushiriki uchaguzi mdogo ujao wa eneobunge hilo.

Wanasiasa kadhaa tayari wametangaza azma ya kutaka kuwania kiti hicho, kilichoachwa wazi baada ya Murunga kufariki mwezi Novemba.Bi Murunga ni miongoni mwa wawaniaji ambao wameidhinishwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa kama wagombea huru.

Hao ni pamoja na mwenyekiti wa Hazina ya Ustawi wa Eneobunge (NG-CDF) la Matungu, Bw Athman Wangara Khamisi, na meneja wa eneobunge hilo Bw Odanga Mutimba Pessa. Aliyekuwa kiongozi wa vijana ngazi ya kitaifa katika chama cha Ford Kenya, Bw Bernard Wakoli, pia ameidhinishwa kuwa mgombea huru.

Bw Wakoli aligura Ford Kenya baada ya kiongozi wa chama hicho Moses Wetang’ula kutangaza kwamba watamuunga mkono mwaniaji wa Amani National Congress (ANC).

Wawaniaji huru wengine watakaoshiriki uchaguzi huo mdogo wa Machi 4, 2021, ni Samuel Munyekenye, Wilberforce Chitechi Luttah, Notcus Borry Kevin na Stanslaus Kubende.

Vile vile, kutakuwepo Bw Charles Lutta Kasamani ambaye alikuwa akijiandaa kushiriki mchujo wa ANC lakini akagura baada ya uongozi wa chama kumpa tiketi ya moja kwa moja Bw Peter Nabulindo.

Murunga alichaguliwa kupitia tiketi ya ANC katika Uchaguzi Mkuu wa 2017 na alikuwa amehudumu kwa miaka mitatu kabla ya kukumbana na mauti.

 

You can share this post!

DPP apewa mwezi mmoja kuamua ikiwa atamshtaki upya Wambua

Polisi kuimarisha doria sherehe za Krismasi