Siasa

Mkutano wa mahakama na Rais utazaa haramu – Raila

January 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA RUSHDIE OUDIA

KIONGOZI wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga amemtaka Jaji Mkuu Martha Koome aachane na jitihada zake za kukutana na Rais William Ruto akisema hatua hiyo itasambaratisha nguvu za idara ya mahakama na taifa kwa ujumla.

“Kuna kesi dhidi ya asasi ya urais ambazo zingali mahakamani hivyo huu si wakati mwafaka wa Jaji Mkuu Koome kukutana na Rais,” amesema Bw Odinga akiwa katika Sosa Villages, Kaunti ya Vihiga ambapo amekutana na wajumbe wa ODM.

Bw Odinga ambaye pia ni kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) amesema Rais na utawala wake ni sharti kuheshimu sheria na hakuna nafasi ya Bi Koome kujidunisha kwa ‘kulala kitanda kimoja na asasi nyingine ya serikali’.

Viongozi wengine ambao wamekosoa pendekezo hilo ni Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, na Mwenyekiti wa ODM John Mbadi (mbunge maalum).

Badala yake, viongozi hao wamesema mazungumzo ya aina hiyo yanafaa kuwa ya kitaifa yanayohusisha Wakenya wote.