• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Mnatoza ushuru na hamlipi madaktari, Kalonzo aishangaa serikali

Mnatoza ushuru na hamlipi madaktari, Kalonzo aishangaa serikali

NA WYCLIFFE NYABERI

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka ameitaka serikali ya Kenya Kwanza kuwalipa madaktari ili wasitishe mgomo wao.

Bw Musyoka alishangaa utawala wa sasa unatoza ushuru mwingi hivyo hakuna kisingizio kwamba hakuna rasilimali za kutosha.

Alisema hayo Alhamisi akiwa katika mji wa Nyamira

Alidai Rais William Ruto ni kama analemewa na majukumu yake.

“Madaktari wanagoma takribani wiki mbili sasa. Wamelemeza huduma za afya. Wamesimama kidete na wanafunzi wa udaktari ambao wamemaliza masomo yao lakini hawajaajiriwa kazi. Badala ya Rais kuwapa kazi, anatumia fedha hizo kuongeza mgao katika afisi yake,” Bw Musyoka akasema.

Aliongeza, “Tunahitaji madaktari ili wagonjwa wapate huduma bora za afya katika vituo vyetu.”

Makamu huyo wa zamani wa rais alisema wakati umefika wa kuikomboa nchi kutoka kwa minyororo ya viongozi wa kujipiga gamba, ambao wanafanya maisha ya Wakenya kuwa ya kusikitisha.

“Wakati huu, hakuna kurudi nyuma. Ikiwa hutapunguza ushuru, tutahamasisha Wakenya wote na watakung’oa mamlakani baada ya kuhudumu kwa muhula mmoja pekee.

Bw Musyoka, ambaye alifungua afisi za chama chake katika kaunti za Kisii na Nyamira, aliwataka wafuasi wake kujisajili kwa wingi.

Kiongozi huyo wa Wiper alimweleza Rais kuwa na wasiwasi kwa kudai kwamba hata eneo la Mlima Kenya, ambalo lilimpigia kura nyingi katika uchaguzi mkuu wa 2022, lilikuwa limepoteza imani na utawala wake.

“Hata watu wa Mlima Kenya wamepoteza imani nao. Wameona walitumika. Waliwaweka mamlakani bila kujua wao ni nani. Walikuwa mbwa mwitu waliovaa ngozi ya kondoo,” akasema.

Kiongozi wa Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa naye alisema hakuna jinsi serikali ingesema haina pesa za kuheshimu Mkataba wa Makubaliano ya Pamoja (CBA) ilhali rais yuko tayari kutenga pesa za kuwatunuku marafiki zake ambao walibwagwa kwenye uchaguzi wa 2022 nafasi za unaibu waziri (CASs).

“Hakuna jinsi utasema huna pesa za kuwalipa madaktari, ilhali unataka kuwatunuku waandamizi wako walioshindwa katika uchaguzi wa 2022. Wakenya katika kaunti zote 47 wanateseka,” waziri huyo wa zamani alisema.

Aliongeza, “Hakuna jinsi huwezi kuwalipa madaktari ilhali unaongeza bajeti ya Ikulu na kutenga hadi Sh4 bilioni kwa chai. Ni chai ya aina gani itatumia pesa hizo zote?” Bw Wamalwa aliuliza.

“Huwezi kuendelea kuwabebesha Wakenya ushuru wa juu mchana na usiku. Umeongeza VAT maradufu kwa bidhaa za kimsingi. Sasa wanalenga mkate wa ushuru na maziwa. Sasa ni wakati wa kusema imetosha,” Bw Wamalwa alisema.

Huku kinara wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga akitangaza mipango ya kuwania Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Bw Kalonzo na Bw Wamalwa wamekuwa wakizunguka nchi nzima ili kujiweka mbele zaidi katika Uongozi wa muungano huo.

Wawili hao walianza ziara yao ya siku tatu katika eneo la Nyanza Kusini mnamo Jumatano huko Kehancha na wataimaliza Ijumaa.

  • Tags

You can share this post!

Muziki: Wito kizazi cha sasa Kenya kiige kina Nameless, Jua...

Masharti ya Agikuyu kumkubali Gachagua kuwa msemaji wao

T L