• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 11:46 AM
Msaidizi wa Raila ajiunga na UDA

Msaidizi wa Raila ajiunga na UDA

NA CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA msaidizi wa kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga, Silas Jakakimba, amejiunga rasmi na chama cha Rais William Ruto, United Democratic Alliance (UDA).

Hii ni baada ya mwanasiasa huyo kugura ODM mwaka 2023 baada ya kutofautiana na Bw Odinga, kisiasa.

Bw Jakakimba ambaye aliwania ubunge wa Suba Kaskazini na akashindwa na Bi Millie Odhiambo Mabona katika uchaguzi mkuu wa 2022, alipata mapokezi mazuri katika makao makuu ya UDA, Nairobi mnamo Jumanne kutoka kwa Katibu Mkuu wa wa chama hicho Cleophas Malala.

“Leo niko hapa kutangaza kuwa nimejiunga rasmi na chama cha United Democratic Alliance,” akasema Bw Jakakimba.

Bw Jakakimba alisema kuwa hatua hiyo ni ithibati ya umaarufu wa chama hicho katika eneo la Nyanza na sehemu mbalimbali nchini.

“Nataraji kuungana na watu wengi katika eneo la Nyanza ambao sasa wako tayari kujiunga, kuvumisha na hata kuwania viti mbalimbali kwa tiketi ya UDA, ” akasema mwanasiasa huyo ambaye amehudumu kama msaidizi wa Bw Odinga kwa zaidi ya miaka 19.

Hata hivyo, Bi Odhiambo alipuuzilia mbali hatua ya Bw Jakakimba kujiunga na UDA akisema haiwezi kuyumbisha ushawishi wa ODM eneobunge la Suba Kaskazini na eneo la Nyanza kwa ujumla.

“Bw Jakakimba ni mtu anayeongozwa na tamaa ya kujifaidi kibinafsi wala sio wakazi wa eneo hili au Nyanza kwa ujumla. Ningependa kumhakikishia kuwa ODM ingali na nguvu Suba Kaskazini, Nyanza na Kenya kwa ujumla,” akasema Bi Odhiambo katika taarifa fupi kwenye ukurasa wa akaunti yake katika mtandao wa X.

  • Tags

You can share this post!

Mradi wa Dongo Kundu kuendelea baada ya muafaka

Urais Senegal: Faye amlemea mgombea wa ‘deep...

T L