Msipochunga, asilimia 56 yenu hamtarudi bungeni, Wetang’ula aambia wabunge
SPIKA wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, amekemea vikali kamati za Bunge kwa kile alichokitaja kuwa tabia ya kuwahangaisha maafisa wa serikali kwa kuwaita mara kwa mara kutoa maelezo na mialiko inayorudiwa, akionya kuwa mwenendo huo unadhoofisha utendaji wa taasisi za umma na kuchelewesha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa kikao cha Bunge la Kitaifa cha kuweka ajenda ya mwaka 2026 mjini Naivasha, Spika alisema Bunge liko katika kipindi nyeti, takriban miezi 17 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027, hali inayohitaji wabunge kujitathmini na kujikita katika majukumu yao ya kikatiba.
“Huu ni wakati wa kutafakari na kujirekebisha. Lazima tukumbuke wajibu wetu wa kudumu wa kutunga sheria, kusimamia serikali na kuwakilisha Wakenya kwa heshima na dhamira,” alisema Wetang’ula.
Spika alionya kuwa joto la siasa linapoongezeka kuelekea uchaguzi, kamati hazipaswi kuruhusu ushindani wa kisiasa kuathiri heshima, mshikamano na sifa za Bunge. Alisema mamlaka ya Bunge hayatokani tu na sheria zinazopitishwa bali pia mwenendo wa wabunge.
“Bunge halihukumiwi kwa idadi ya sheria linalopitisha pekee, bali kwa athari za sheria hizo kwa maisha ya wananchi na uthabiti wa taasisi tunazoacha nyuma,” alisema.
Akikemea namna kamati zinavyotekeleza jukumu la usimamizi, Wetang’ula alisema kumekuwa na visa ambapo wakuu wa taasisi kama Inspekta Jenerali wa Polisi na Tume ya Huduma kwa Walimu wameitwa mbele ya kamati tofauti kuhusu masuala yanayofanana.
“Usimamizi ni jukumu la kikatiba, lakini haupaswi kuunda taswira ya shinikizo lisilofaa au kusababisha kulemaa kwa shughuli za utawala,” alionya, akizitaka kamati ziratibu kazi zao na kuepuka urudufu.
Alisisitiza kuwa kamati za ukaguzi, hasa Kamati ya Hesabu za Umma (PAC) na Kamati ya Uwekezaji wa Umma (PIC), lazima zikamilishe kazi zao kwa wakati kwa mujibu wa Katiba.
“Nasisitiza tena mwongozo wangu kwa kamati za ukaguzi, hususan Kamati ya Hesabu za Umma (PAC) na Kamati ya Uwekezaji wa Umma (PIC), kuhakikisha kuwa zinakamilisha kazi zao kwa wakati unaofaa. Kuhusu kamati za ukaguzi, muda wa kikatiba chini ya Kifungu cha 229(8) cha Katiba wa kuzingatia na kutoa maamuzi kuhusu ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ni miezi mitatu tangu ripoti hiyo kuwasilishwa Bungeni. Hatuna budi kufanya kazi kwa busara, haraka na kwa kuzingatia muda uliowekwa kikatiba,” alisema.
Wakati huohuo, Spika aliwakumbusha wabunge kuhusu uhalisia wa siasa za Kenya, akisema takriban asilimia 56 ya wabunge wa sasa huenda wasirejee Bungeni baada ya uchaguzi ujao.
“Siasa zina mvutano na uhalisia ni jambo lisiloepukika. Ndio maana urithi wa taasisi hii ni muhimu kuliko mustakabali wa mtu binafsi,” alisema Wetang’ula.
Aliwataka wabunge kutumia muda uliosalia kuacha alama kupitia sheria bora, usimamizi wa kimkakati na uwakilishi unaolenga maslahi ya wananchi, akisisitiza kuwa historia itawahukumu kwa mchango wao, si kelele za kisiasa.