Msithubutu kuweka wawaniaji katika ngome zetu, ODM yaonya UDA
HATUA ya ODM kutaka UDA isiwe na wawaniaji katika ngome zake za kisiasa 2027 imeibua mgawanyiko mpya ndani ya Serikali Jumuishi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Japo ODM imeonyesha kila ishara ya kumuunga mkono Rais William Ruto mnamo 2027, imeonya UDA dhidi ya kuingilia ngome zake za kisiasa za Nyanza, Magharibi na Pwani.
Nia ya ODM ni kuhakikisha kwamba inasalia na wabunge wengi ili kuipa jukwaa bora la kuwa na ushawishi kwenye muungano na Rais Ruto baada ya 2027.
Umaarufu wa ODM kwenye ngome zake za Gusii na Magharibi nao sasa unatishiwa na vyama vya UPA na DAP-Kenya mtawalia.
Baadhi ya wanachama wa ODM pia wameonyesha dalili za kuhama wakihofia kuwa watachezewa shere katika mchujo wa 2027.
Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga ambaye pia ni gavana wa Homa Bay alitoa pendekezo la UDA kutokanyaga ngome za ODM kupitia uwaniaji mnamo 2027.
“Tuko kwa Serikali Jumuishi kama ODM na kati ya makubaliano yetu ni kuwa hakuna kuingiliwa kwa ngome zetu,” akasema Bi Wanga akizungumza Awasi, eneobunge la Nyando mnamo Ijumaa.
Kauli hiyo imewakasirisha baadhi ya viongozi wa ODM wanaoona kuwa watachezewa shere kwenye uteuzi na pia viongozi wa UDA hasa kutoka kaunti za Nyanza ambapo ODM imetawala kisiasa.
Gavana wa zamani wa Nairobi Evans Kidero aliye mwanachama wa UDA jana aliambia Taifa Leo kuwa watapambana na kupinga juhudi zozote za kuzuiwa kuwania Nyanza.
Dkt Kidero alisema watu wanastahili kupewa nafasi ya kuwachagua viongozi wanaowataka badala ya kulazimishiwa na chama.
Alisema njia pekee ambayo eneo hilo linaweza kuthamini siasa za marehemu Raila Odinga ni kukumbatia demokrasia.
“Kutengea chama eneo kisha kuvizuia vingine kuwasilisha mwaniaji ni ukiukaji wa demokrasia. Hatutakubali hilo,” akasema Dkt Kidero.
Mwenyekiti wa UDA Kaunti ya Homa Bay Kennedy Obuya naye alisema chama hicho kitakuwa na wawaniaji kwenye ngazi zote za uongozi Luo Nyanza ili raia wawe na hiari ya kuwachagua viongozi ambao wanawataka.
“UDA itakuwa na wawaniaji Kisumu, Siaya, Homa Bay na Migori. Watu wetu watakuwa na jukumu la kuwachagua viongozi na wafahamu kuwa hakuna Serikali Jumuishi bila UDA,” akasema Bw Obuya.
Kwenye uchaguzi mdogo wa Kasipul mwezi uliopita, ODM ilishutumiwa kwa kuandaa mchujo uliopendelea Boyd Were mwanawe aliyekuwa Mbunge wa eneo hilo marehemu Ong’ondo Were.
Hata kabla ya chama kuandaa mchujo wake, baadhi ya viongozi wake wakuu walikuwa wakipambana Bw Boyd apokezwe tikiti.
Jana, Naibu Kiongozi wa ODM Godfrey Osotsi aliwahakikishia wafuasi wa chama kuwa kitasalia imara kuelekea 2027.
“Kuna watu wengi wanafikiria ODM itapasuka bila Raila. Watashangaa lakini lazima tuongee na wenzetu ili tufahamu tutapata nini baada ya uchaguzi wa 2027,” akasema Bw Osotsi.
“Nilisikia baadhi ya viongozi wakisema Waluhya waondoke ODM. Sisi maslahi yetu lazima yalindwe chamani na viongozi wanastahili kukoma kusawiri ODM kama chama cha Waluo au Nyanza pekee,” akasema Bw Osotsi.
Mbunge wa Uriri Mark Nyamita wiki jana alisisitiza kuwa ni uteuzi huru ndio utasaidia ODM kuendelee kuwika katika ngome zake. Mbunge huyo analenga kutumia ODM kuwania ugavana wa Migori mnamo 2027.
Naye Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi ashatangaza kuwa hatatetea kiti chake kupitia ODM kwa sababu ana hakika uteuzi wa chama hautakuwa huru na utaingiliwa.