Mswada wa Fedha: Spika Weta awasuta wabunge kwa kulialia hadharani
NA JESSE CHENGE
SPIKA wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula amewasihi Wabunge, hasa wa upinzani, kuacha kulialia kuhusu Mswada wa Fedha wa 2024 mazishini na sherehe nyingine za umma na badala yake wawasaidie wananchi kuuelewa vyema.
Kiongozi huyo wa chama cha Ford Kenya alitoa kauli hiyo Jumatano katika eneobunge la Kabuchai, Kaunti ya Bungoma, wakati wa mazishi ya Mzee Yonah Namuli ambaye alikuwa mzee maarufu wa kuendeleza mila na desturi za Wabukusu.
Hata hivyo, Spika Wetang’ula aliwataka Wabunge kutumia likizo ya mwezi mmoja kutafakari kuhusu mswada huo wa fedha na kutaka kamati katika Bunge la Kitaifa kuandaa bajeti.
Wakenya wamelalamika pakubwa baada ya Mswada wa Fedha wa 2024 kupendekeza ushuru wa ziada ya thamani (VAT) ya asilimia 16 kwa mkate, kumaanisha bei ya mkate wa gramu 400 utapanda kwa Sh10. Kwa sasa bei ya mkate huo ni Sh65.
Pia mswada huo unapendekeza ushuru mpya wa asilimia 2.5 ya thamani ya gari ambao wamiliki watakuwa wakilipa kila mwaka. Kiwango cha chini ni Sh5,000 na kiwango cha juu zaidi ni Sh100,000.
“Ninyi ndio mlio na wajibu wa kuwasilisha mapendekezo ya bajeti kupitia kamati zenu. Tafadhali acheni kusimama mbele ya umma na kulalamika kuhusu mswada wa fedha ilhali ninyi ndio mnaoandaa bajeti hiyo,” alisema spika Wetang’ula.
Aliwarai wabunge kuketi chini na kufanya mambo yanayoweza kuwanufaisha raia.
“Wapigakura wanawategemea na kuwa na imani kwenu kwa sababu waliwachagua muwafanyie kazi,” akasema.
Spika pia aliwataka wakazi wa Bungoma kusaidia serikali ya Rais Ruto kwa kuelezea miradi ya maendeleo inayoendelea katika Kaunti ya Bungoma.
Bw Wetang’ula alitaja ujenzi unaoendelea wa Soko la Chwele kwa kima cha Sh300 milioni, ujenzi wa soko la Chebukube na soko la Kamukunywa katika eneo la Kimilili kuwa ni miongoni mwa miradi ambayo inatekelezwa na serikali ya Kenya Kwanza.
Aidha alitaja ukarabati wa barabara ya Malaba-Kanduyi ambapo itafanywa kuwa barabara ya kiwango cha kimataifa.
“Malori yanayosafiri kutoka Uganda kujiunga na barabara ya Kanduyi yameiharibu barabara hiyo na ndio maana Rais ameamuru ukarabati wake,” akasema.
Aidha, Bw Wetang’ula alisema serikali itatoa Sh25 milioni kwa ajili ya upanuzi na ujenzi wa tawi la Chuo cha Mafunzo ya Matibabu Nchini (KMTC) katika eneobunge la Kabuchai.
Matamshi ya Wetang’ula yaliwiana na ya Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa ambaye alilaumu baadhi ya wabunge ambao wamekuwa mstari wa mbele kupinga mswada wa fedha, akisema ni wakati wao kuwasilisha mapendekezo.
“Badala ya kusumbua na kutokubaliana kuhusu mswada wa fedha kama viongozi kutoka eneo hili, tunapaswa kujiweka katika jamii ya eneo la Magharibi na kuanza majadiliano kuhusu jinsi tutakavyopata sehemu kubwa ya bajeti itakayokuja,” akasema Bw Barasa.
Kwenye mazishi hayo, walikuwepo Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka, Naibu Gavana Pasta Jenipher Mbatiany, mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Bungoma Catherine Wambilianga na wakilishi wa wadi kadhaa za Kauti ya Bungoma.